Na: Mwandishi Wetu, Tanga.
Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Mwalimu Novemba 21,2024, ameanza kwa kishindo kuwanadi wagombea wa mitaa mitatu ya kata tatu ndani ya jimbo la Tanga Mjini.
Katika mikutano yake mitatu tofauti, Ummy Mwalimu aliwasihi wananchi kuwaamini wagombea waliopitishwa na CCM kugombea mitaa mbalimbali ya jimbo la Tanga Mjini ili kuweza kuwakilishwa vyema katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Wagombea aliowanadi ni wale wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Mitaa ya Mwakidila 'B' (Kata ya Tangasisi), Sahare Kijijini (Kata ya Mzingani) na Sokoni (Kata ya Ngamiani Kati).
Ummy amesema kero na changamoto mbalimbali zitatatuliwa na wagombea watokanao na CCM kwani CCM ndiyo chama chenye wagombea bora na chenye muunganiko mzuri wa kiuongozi kuanzia ngazi ya juu hadi chini.
Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu aliwakumbusha wananchi hao kazi nzuri na kubwa zilizofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa katika Jimbo la Tanga Mjini ambazo zimegusa pia mitaa na kata zao.
Vilevile, Ummy Mwalimu amesema wananchi wa Tanga Mjini wanalo deni Kwa Rais Samia kutokana na kuleta miradi mingi ya maendeleo Tanga Mjini, huku akiwakumbusha njia pekee ya kumshukuru Rais Samia ni kuwachagua wagombea wote wanaotokana na CCM.
Aidha, Ummy Mwalimu aliwasihi wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi siku ya Tarehe 27 Novemba, 2024 kupiga kura ili CCM iweze kupata ushindi wa kishindo.
Mkutano huu ni mwendelezo wa kampeni zilizozinduliwa Novemba 20, 2024 na Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Hemed Suleimani Abdullah.
No comments:
Post a Comment