Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesisitiza utafiti uendelee kufanyika kubaini maeneo yenye maji ya uhakika ili visima vichimbwe kwa ajili ya kuondoa adha ya maji inayowakabili wakazi wa Jiji la Dodoma hususani kata ya Nkuhungu.
Pia amewataka Watendaji wa Sekta ya Maji kutoingiza siasa katika maisha ya watu kwani maji ni uhai,kwani jukumu la Wizara ya Maji na taasisi zake ni kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika.
Aweso ameyasema hayo Leo Oktoba 31,2024 wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi ya Nkuhungu, akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde.
Aweso ameitaka DUWASA kuhakikisha wanazingatia mgao wa maji kwa wananchi kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji kulingana na ratiba iliyowekwa.
Pia amewahakikishia Wakazi wa Kata ya Nkuhungu suala lao la kupata maji linashughulikiwa kwani kuna vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa na Serikali hivyo vitaanza kazi Nkuhungu kwa wakati.
Pia amepiga marufuku suala la kuwakatia maji wananchi siku za wikiend au Sikukuu kwani ni kinyume cha Sheria.
Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma mjini na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amewahakikishia wakazi wa Kata ya Nkuhungu na maeneo mengine ya jijini Dodoma dhamira yake ya kuendelea kushughulikia changamoto ya maji ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi.
Mhe. Mavunde amemshukuru Waziri wa Maji kwa jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma za uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa Jiji ikiwa ni mpango wa utatuzi wa adha ya maji katika jiji la Dodoma.
No comments:
Post a Comment