Mkugurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya ametangaza uzinduzi huo kufanyika tarehe 25 Novemba 2024 Mkoani Manyara.
Simbaya amesema UTPC kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Manyara, Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Manyara (MNRPC) pamoja na wadau wengine wamejipanga kuzindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ambapo mara baada ya uzinduzi kampeni zitahamia kwenye vyombo vya habari pamoja na majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
Aidha ameeleza umhimu wa kushiriki katika kampeni za kutokomeza ukatili wa kijinsia kuwa si tu inajenga jamii iliyostaarabika bali inachangia lengo la maendeleo endelevu namba tano ambalo linalenga kufanikisha usawa wa jinsia na kuwezesha wanawake na wasichana wote ifikapo mwaka 2030.
“Suala la unyanyasaji wa kijinsia ni suala la kimaendeleo kwa sababu unyanyasaji upo katika mapana na marefu sana kwahiyo tunaposhiriki kupinga unyanyasaji wa kijinsia wa aina yoyote ile maana yake tunashughulika na suala muhimu ambalo tukifanikiwa tutasukuma kwa kiasi kikubwa sana maendeleo ya nchi yetu na dunia nzima kwa ujumla” amesema Kenneth Simbaya.
Ameongeza kuwa “suala la kijinsia ni suala mtambuka hivyo watu wakipewa elimu tutafanikiwa kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia”
Hilda Kileo ni Ofisa Programu, Utawala na Maendeleo ya Klabu kutoka UTPC ambaye pia ni mratibu wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia amesema lengo la kufanya uzinduzi huo katika mkoa wa Manyara ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya ukatili kwa kuwa mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwepo na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia.
Kadhalika amebainisha kuwa kampeni hizo zitaendeshwa kwa siku zote 16 kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, “X space (twitter)” huku mtandao wa “WhatsApp” ukitajwa kuwa jukwaa muhimu litakalotumika zaidi kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili kwa kina kuhusu kiini cha ukatili wa kijinsia na mbinu za kulikabili janga hilo.
No comments:
Post a Comment