Na Mwandishi wetu
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa gari jipya la kuhudumia wagonjwa lenye usajili wa STN 3638 kwa Kituo Cha Afya cha Migoli ili kuendelea kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi (Mb) Isimani amemkabidhi gari hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bwn. Robert Masunya leo tarehe 24/11/2024 wakati wa ziara ya kikazi katika vijiji vya Kinyari Mbweleli, Makatapora, Mtera na Migoli.
Amefafanua kwamba Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kazi yake ni kuleta vitu na kujenga miundo mbinu kwa ajili ya kuhudumia wananchi wote hivyo hatuna budi kumshukuru na kumpongeza kwa kazi njema.
Waziri alisema, “Kazi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha wananchi wanaishi maisha bora kitu ambacho kinaonesha utekelezaji wa ilani ya chama kwa vitendo.”
Aidha Waziri Lukuvi, amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji kuweka msawazo mzuri wa ikama ya watumishi wa kada ya afya kwa kuleta Daktari katika Kituo hicho cha Afya Migoli baada ya Mganga aliyekuwepo kwenda masomoni.
Ameeleza kwamba “Kituo cha Afya Migoli si Kituo cha Afya cha kawaida, tunahitaji upasuaji ufanyike katika kituo hiki, ikiwemo kukamilisha wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, na ujenzi wa vyoo vya nje kwa jengo la wagonjwa wa nje kwa sababu Serikali imeshatenga fedha kwenye bajeti.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Bwn. Robert Masunya amesema gari la wagonjwa walilopokea litasaidia katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Migoli na wananchi wanaopita njia ya Dodoma Iringa na ameahidi kuhakikisha gari hilo linatunza vizuri.
“Tunaujenzi unaotakiwa kukamilika katika kituo hicho cha afya na majengo mengine yanayotakiwa kujengwa ili yaweze kusaidia kutoa huduma, tumejipanga kama Halmashuri kuhakikisha kila kitu kinakamilika kwa wakati,” alisema
Naye ndg. Adphonce Mbasu mwananchi wa kinyari amesema ujio wa gari la wagonjwa utasaidia katika kurahisisha utoaji wa huduma za dharura kwa wananchi kwa kusaidia wagonjwa wa dharura wanafika katika kituo cha afya kwa wakati na kupokea huduma.
“Gari la wagonjwa limepunguza Kadhia ya kutembea umbali mrefu kwa wagonjwa wa dharura ili kupata huduma ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za kukodi usafiri binafsi,” alieleza
No comments:
Post a Comment