WAZIRI MKUU AKAGUA MUENDELEZO WA ZOEZI LA UOKOAJI KARIAKOO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 18, 2024

WAZIRI MKUU AKAGUA MUENDELEZO WA ZOEZI LA UOKOAJI KARIAKOO


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Novemba 18, 2024 amekagua muendelezo wa zoezi la uokoaji katika jengo lililoporomoka Novemba 16 Kariakoo Jijini Dar es salaam, ambapo amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu hadi atakapookolewa mtu wa mwisho.

Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanamtafuta mmiliki wa jengo hilo ili aweze kuisaidia timu kufahamu juu ya chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo. Pia, amesema hadi sasa jumla ya watu 86 wameokolewa kati yao watano wanaendelea na matibabu, pamoja na hao 16 wamefariki.

Aidha, ametoa wito wa Watanzania kuacha kuchangisha wananchi kwani Serikali inautaratibu wa utoaji wa misaada kupitia Kamati ya Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na akaunti hiyo iko BOT. “Yuko binti anaitwa Niffer (Jenifer Jovin) atafutwe aeleze nani alimpa kibali cha kuchangisha umma, amekusanya shilingi ngapi, amezipeleka wapi na kwa nini amefanya hivyo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wakati zoezi la uokoaji likiendelea tayari Serikali imeunda timu ya watu 19 ya uchunguzi ikiwa ni utekezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia la kufanya ukaguzi wa chanzo cha kudondoka kwa jengo hilo. “Timu hii pia itakagua uimara wa majengo yote yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa katika eneo lote la Kariakoo.”

Baada ya kukagua zoezi la uokoaji katika eneo la Kariakoo, Mheshimiwa Majaliwa aliongoza zoezi la kuaga miili 15 kati ya 16 waliofariki hadi sasa kutokana na ajali ya kuporomoka kwa jengo iliyotokea Jumamosi Novemba 16, 2024 saa tatu asubuhi. Amesema Serikali inagharamia matibabu kwa majeruhi wote pamoja na huduma ya mazishi kwa marehemu wa ajali hiyo.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi alisema Serikali inaendelea kuratibu shughuli za uokoaji ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za haraka ili kusaidia zoezi hilo.

Amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imeendelea kuratibu mazoezi ya utafutaji na uokoaji, kutoa huduma ya kwanza na kuwafikisha hospitalini, kutoa huduma za kijamii pamoja na kuwezesha mitungi ya gesi ya oksijeni kwa ajili ya watu walioko chini ya kifusi.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiasha wa Kariakoo, Martine Mbwana alitumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa ujumla kwa hatua alizozichukua na msaada walioutoa tangu kutokea kwa ajali hiyo hadi sasa.



No comments:

Post a Comment