
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
SERIKALI imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuwezesha kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua inayolenga kuwawezesha vijana kujiajiri, kuajiri wengine na kutoa huduma bunifu katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo Februari 4, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta hiyo.
Mhe. Kairuki amesema Serikali imejikita kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanaboresha maisha ya wananchi wa kawaida mijini na vijijini, kwa kuongeza upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kidijitali na fursa za kiuchumi.
Amefafanua kuwa fedha hizo zitatumika kusaidia kampuni changa za TEHAMA kuendeleza bunifu zitakazotumika katika sekta muhimu ikiwemo afya, elimu, kilimo, fedha na biashara, hivyo kuchochea uchumi wa kidijitali unaojumuisha wananchi wengi zaidi.
Katika kuimarisha uwajibikaji na uwazi wa utoaji huduma za umma, Waziri amesema taasisi 800 za Serikali zimeunganishwa kwenye Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali (GovNet), hali inayowawezesha wananchi kuwasilisha kero zao kwa njia ya kidijitali na kupata majibu kwa wakati.
Aidha, upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano umeendelea kuboresha maisha ya wananchi vijijini baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano katika kata 713, hatua iliyoongeza upatikanaji wa huduma za simu, intaneti pamoja na huduma za kifedha kwa njia ya simu.
Mhe. Kairuki amesema Serikali pia imeendelea kudhibiti gharama za mawasiliano, ambapo bei ya kupiga simu ndani ya nchi imeendelea kubaki Shilingi 29 kwa dakika, jambo linalowezesha wananchi wengi zaidi kumudu huduma za mawasiliano.
Katika kuimarisha upatikanaji wa taarifa na huduma za Serikali kwa wananchi, Wizara imeendelea kupeleka huduma ya Wi-Fi katika maeneo ya umma ikiwemo masoko, hospitali, stendi za mabasi na vyuo, hatua inayochochea matumizi ya intaneti na huduma za kidijitali nchini.
Amesema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinazolenga kujenga Taifa la kidijitali lenye uchumi shindani na unaowanufaisha wananchi wote.

No comments:
Post a Comment