TUU YAHIMIZA HAKI NA WAJIBU VIENDE SAMBAMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 10, 2026

TUU YAHIMIZA HAKI NA WAJIBU VIENDE SAMBAMBA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA


Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma (TUU), Nolasco Jacob Kipanda, amesema Tume itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa waajiri, watumishi wa umma na mamlaka za nidhamu ili kupunguza migogoro ya kiutumishi na malalamiko yanayotokana na kutokuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Kipanda amesema malalamiko mengi yanayofikishwa mbele ya Tume yangeweza kuzuilika endapo kungekuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na taratibu za utumishi wa umma, akisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kudai haki zake kwa wakati huohuo akitimiza wajibu wake ipasavyo mahali pa kazi.

Aidha, amewataka waajiri na mamlaka za ajira kushughulikia masuala ya ajira na nidhamu kwa kuzingatia sheria, kuwasilisha taarifa kwa Tume kwa wakati na kutekeleza maagizo yanayotolewa ili kuimarisha uwajibikaji na utawala bora katika utumishi wa umma.

Akizungumza kuhusu maamuzi ya Mkutano wa Nne wa Tume kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema Tume ilipokea na kutolea uamuzi jumla ya rufaa na malalamiko 76, zikiwemo rufaa 57 na malalamiko 19, yaliyosikilizwa katika mkutano uliofanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 3, 2026 jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Mst.) Hamisa H. Kalombola.

Mbisso amesema ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma na taaluma, utoro kazini, kushindwa kutekeleza majukumu na uzembe uliosababisha hasara kwa mwajiri ni miongoni mwa makosa yaliyojitokeza zaidi katika rufaa zilizowasilishwa mbele ya Tume.

Ameongeza kuwa malalamiko mengi yaliyopokelewa yalihusu kutolipwa stahili, kuondolewa katika utumishi wa umma bila kuzingatia sheria, kusitishwa kwa mikataba ya ajira bila kufuata utaratibu wa kisheria, kutopandishwa cheo na uhamisho usiozingatia taratibu.

Kwa mujibu wa Mbisso, warufani tisa na warufaniwa wawili waliomba kuruhusiwa kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zilizokuwa mbele ya Tume, huku mamlaka moja ya nidhamu ikiitwa kutoa maelezo kuhusu namna ilivyoshughulikia shauri la kinidhamu la mtumishi aliyekuwa chini yake.

Amesema pia Tume ilifanya ziara za kikazi katika taasisi tano za Serikali jijini Mwanza kwa lengo la kutoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira, mamlaka za nidhamu na watumishi kuhusu uzingatiaji wa sheria, haki na wajibu wao katika utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment