MHANDISI SEFF ATOA WITO KWA WANANCHI KUACHA KUTUPA TAKATAKA KWENYE MITARO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 9, 2024

MHANDISI SEFF ATOA WITO KWA WANANCHI KUACHA KUTUPA TAKATAKA KWENYE MITARO


🎈🎈Awataka Maafisa Mazingira na Maendeleo ya Jamii wa TARURA kutoa elimu kwa wananchi.  

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff ametoa wito Kwa wananchi kutunza miundombinu ya barabara na kuacha tabia iliyojengeka ya kutupa hovyo takataka kwenye mitaro. 

Wito huo ameutoa kufuatia ziara yake aliyoifanya jijini Dodoma ikilenga kukagua Miundombinu ya Barabara iliyoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni jijini humo. 

"Tumepita maeneo mengi, tumeona wananchi wanatupa hovyo takataka, mfano wafanyabiashara wa maduka wanatupa takataka kwenye mifereji mbele ya maduka yao na madhara yake ni kwamba mvua ikija maji badala ya kupita kwenye mifereji yanapita juu ya barabara na kuleta uharibifu mkubwa utakaopelekea matumizi mengine ya fedha kwaajili ya kurekebisha uharibifu huo" 

" Sisi tuna Kitengo cha Masuala ya Jamii katika ngazi ya Makao Makuu lakini pia na kwa baadhi ya mikoa, kwa hiyo niwasisitize hawa nao waendelee kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kuzuia utupaji wa takataka kwenye mitaro." amefafanua Mhandisi Seff.

Aliongeza kusema kuwa wanayo Kampeni ijulikanayo kama 'Mitaro Sio Jalala' na kwa mujibu wa Mhandisi Seff, Kampeni hiyo imeshafanyika katika Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na bado wanaendelea nayo kwa mikoa mingine ili kuwaelimisha wananchi kuwa mitaro wasiigeuze kuwa jalala kwa sababu barabara wanazojenga ni kwa faida yao wananchi na jamii yote ya Tanzania.

Kuhusu mpango wa kujenga Mitaro mikubwa kwa ajili ya kukabiliana na maji ya mvua Mhandisi Seff amesema kuwa walikuwa na Mradi wa TSSP ambapo kupitia Mradi huo walifanikiwa kujenga mitaro mikubwa kwaajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

Ameeleza kuwa kupitia Mradi mwingine unaotekelezwa sasa wa TACTIC wamepanga kujenga Mitaro mikubwa kwa yale maeneo tete ili mvua zinaponyesha maji yawe yanaelekezwa sehemu salama ama kwenye mito au kwenye mabwawa ili kuzuia athari kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment