Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele, amewataka Polisi Kata kuendeleza ushirikiano wa karibu na jamii ili kuliwezesha Jeshi la Polisi kupata taarifa za uhalifu mapema kabla haujatokea.
Akizungumza Machi 2, 2026 katika Bwalo la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lililopo Barabara ya Kilwa, Temeke, Mafwele amesema ushirikiano kati ya Polisi Kata na wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha falsafa ya Polisi Jamii na kudhibiti uhalifu.
Mafwele alizungumza na Polisi Kata 102 kutoka Mikoa ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke katika kikao kilicholenga kuboresha utendaji kazi na kuleta matokeo chanya kwa jamii.
“Niwatake Polisi Kata wote kuzijua vizuri kata zenu kwa kutambua mipaka ya kijiografia, shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo yenu pamoja na makundi yote muhimu yaliyopo. Kupitia ushirikiano na makundi hayo, mtapata taarifa mbalimbali ikiwemo za uhalifu zitakazosaidia Jeshi la Polisi kudhibiti matukio kabla hayajatokea,” amesema Mafwele.
Ameongeza kuwa askari hao wanapaswa kutumia vyema nafasi waliyopewa ya kufanya kazi karibu na wananchi, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga uaminifu pamoja na kufungua fursa za kiuchumi kulingana na mazingira ya maeneo wanayoyahudumia.
CHANZO : MWANANCHI


No comments:
Post a Comment