SERIKALI YAWAONYA MAAFISA RASILIMALIWATU WANAOWAKATAA WATUMISHI WANAOPANGIWA KAZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 17, 2024

SERIKALI YAWAONYA MAAFISA RASILIMALIWATU WANAOWAKATAA WATUMISHI WANAOPANGIWA KAZI



Na Okuly Julius _ Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amekemea vikali tabia ya baadhi ya maafisa rasilimaliwatu nchini wanaowakataa watumishi wanaopangiwa majukumu katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria.

Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo Mtumba jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa idara za utawala na usimamizi wa rasilimaliwatu, ambapo amesema wapo baadhi ya viongozi huwakataa watumishi kwa kuwa hawakutokana na matakwa yao.

"Kwa nafasi zenu kwenye Taasisi mnakotoka ninyi ni jicho la Ofisi ninayoingoza katika kusimamia utekelezaji wa Sera za Utawala, Maadili, Serikali Mtandao, Makazi ya Watumishi wa Umma, Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na Usimamizi wa Rasilimaliwatu," amesema Simbachawene

Simbachawene amesema pamoja na uanzishwaji na utekelezaji wa Mifumo mbalimbali , bado kumekuwa na changamoto ya usimamizi wa Mifumo na kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa watumishi hali inayosababisha Watumishi wa Umma kuendelea kufuatilia masuala mbalimbali ya kiutumishi katika Ofisi ya Rais, Menejiementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikai za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi za Makatibu Wakuu wa Wizara Mama na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa. Baadhi ya changamoto hizo zimejitokeza katika eneo la e-Utendaji, e-Uhamisho na e-Ajira Mbadala.

Ameongeza kuwa pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali , bado Utumishi wa Umma unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuzingatiwa kwa Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yanayosimamia Rasilimaliwatu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya Kiutawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

"Kumekuwa na ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miiko ya kazi katika Utumishi wa Umma ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na Ofisi,"

Na kuongeza kuwa "Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kupokea malalamiko ya watumishi wanaokataliwa kupokelewa katika vituo wanavyohamishiwa au kuajiriwa, upendeleo wa fursa mbalimbali za kiutumishi, kutumia utashi binafsi katika kutafsiri Miongozo inayosimamia haki za watumishi, unyanyasaji wa kijinsia, na ucheleweshaji wa haki na stahiki za kiutumishi,"amesema Simbachawene

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili kwa maafisa hao huku akikemea vitendo vya uvunjifu wa maadili, ikiwa ni pamoja na rushwa na lugha zisizofaa kwa watumishi.

Katika bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Ofisi hii imewapandisha vyeo watumishi 229,159 na kuwabadilisha Kada Watumishi 9,654

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na Mwenyekiti na Mratibu Mkuu wa kikao hicho, Bw. Juma Komi, ameweka wazi lengo la kikao hicho kinachofanyika kwa siku tuta, kuwa ni kujadili na kutathimini nafasi ya wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma na kubadilishana uzoefu wa utendaji na kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali hasa yale yanayohusiana na Utumishi wa Umma.






No comments:

Post a Comment