WADAU WA SEKTA YA UJENZI WAKUTANA KUJADILI MABADILIKO YA SHERIA YA USAJILI WA WAHANDISI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 20, 2024

WADAU WA SEKTA YA UJENZI WAKUTANA KUJADILI MABADILIKO YA SHERIA YA USAJILI WA WAHANDISI


Wizara ya Ujenzi kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imefanya kikao na wadau wa sekta ya ujenzi kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Usajili wa Wahandisi Sura ya 63, kilichofanyika tarehe 20 Desemba, 2024 katika ukumbi wa PSSSF Commercial Complex, jijini Dar es Salaam. Lengo la mabadiliko haya ni kuboresha ufanisi na utekelezaji wa majukumu ya Bodi, pamoja na kuimarisha usimamizi wa sekta ya ujenzi nchini.

Kikao hiki kimewakutanisha wadau muhimu wa sekta ya ujenzi pamoja na wataalam wengineo wakiwemo wataalamu wa sheria ili kutoa mchango wao katika kuboresha vipengele mbalimbali vya sheria hii.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Emmanuel Mapande, amesema kuwa mabadiliko haya ni muhimu sana kwani sekta ya Ujenzi inagusa maisha ya jamii kwa ujumla, hivyo mabadiliko haya yatasaidia kuboresha ufanisi wa wahandisi na kazi za kihandisi nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Wakili Menye Manga, amesema kuwa mabadiliko ya sheria hii ni muhimu ili kuongeza weledi wa wahandisi nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia.

"Tunatazamia sheria itakayozuia wahandisi wasio na maadili na weledi, kwani kuna watu wengi wanaofanya kazi za kihandisi bila kuwa na ujuzi stahiki na weledi," aliongeza Mhandisi Menye Manga.

Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi Bernard Kavishe, amesema kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria ulianza miaka mingi iliyopita na kwamba mnamo Aprili 2022, msajili alianzisha kikosi kazi kilichojumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, timu ya usimamizi ya ERB, Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), wataalamu na wafanyakazi wa ERB, lengo likiwa ni kutambua maeneo yanayohitaji kupitia upya.

Washiriki wa kikao hicho wameipongeza Wizara ya Ujenzi kupitia ERB kwa hatua hii muhimu, inayolenga kuboresha zaidi sekta ya uhandisi nchini.



No comments:

Post a Comment