WAZIRI ULEGA ATOA MAAGIZO YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA KIPANDE CHA UBUNGO HADI KIMARA KUEPUSHA MSONGAMANO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 29, 2024

WAZIRI ULEGA ATOA MAAGIZO YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA KIPANDE CHA UBUNGO HADI KIMARA KUEPUSHA MSONGAMANO


Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ametoa maelekezo ya haraka kuhusu mradi wa upanuzi wa miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT)Awamu ya Kwanza kipande cha Ubungo hadi Kimara, akisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo ili kuepuka msongamano wa magari na hatari zinazoweza kutokea wakati wa dharura.

Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika jiji la Dar es Salaam leo Jumamosi tarehe 28 Desemba, 2024 , Waziri Ulega amesema kuwa barabara zilizojengwa hadi sasa katika kipande cha Ubungo hadi Kimara zina kingo zinazoweza kuzua changamoto kubwa ikiwa kutatokea ajali au dharura yoyote, kwani gari haliwezi kutoka kwa urahisi kwenye barabara.

“Eneo hili tunajenga barabara zetu, lakini ni wazi kwamba kingo zinazowekwa pande za barabara zinapaswa kubadilishwa. Hata katika dharura, gari linapaswa kuwa na uwezo wa kutoka, na hili ni agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Inapotokea ajali au tatizo lingine, kila mtu atakuwa hatarini kwa sababu gari haliwezi kupita,” alisema Waziri Ulega.

Waziri Ulega pia amesisitiza kuwa kama foleni itatokea kutokana na gari kuharibika, itakuwa vigumu kwa magari mengine kupita na kupunguza msongamano, jambo ambalo linaweza kuathiri huduma za jamii.

“Tunayo maelekezo kutoka kwa Rais Samia na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 kwamba kingo za barabara ziachanishwe ili gari liweze kutoka mara moja kama dharura itatokea. Hili ni jambo la msingi, na tunahitaji ubunifu katika utendaji wa miradi hii ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea,” aliongeza Waziri Ulega.

Maelekezo ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega kuhusu kuboresha kingo za barabara ni mfano halisi wa uongozi unaozingatia usalama na ustawi wa wananchi, huku ukiendelea kutatua changamoto za msongamano na dharura barabarani kwa kuhakikisha miundombinu inakuwa salama na rahisi kutumiwa.

No comments:

Post a Comment