HALI YA KIAFYA YA KIJANA HUSSEIN IDD BABU ALIYESAIDIWA MATIBABU NA MHE RAIS SAMIA YAENDELEA KUIMARIKA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, December 29, 2024

HALI YA KIAFYA YA KIJANA HUSSEIN IDD BABU ALIYESAIDIWA MATIBABU NA MHE RAIS SAMIA YAENDELEA KUIMARIKA.



Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA



Hali ya Kiafya ya Kijana Hussein Idd Babu (18) aliyemuomba Mhe Rais Samia Suluhu Hassan msaada wa kupatiwa matibabu inaendelea kuimarika hospitalini Benjamin Mkapa anakoendelea kupatiwa matibabu.

Kijana huyo anaetokea katika kijiji cha Boayi Wilayani Babati Mkoani Manyara alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye kichwa.

Mama mzazi wa Kijana huyo, Bi. Aziza Said Nkolomu amesema tatizo hilo la uvimbe kichwani limemsumbua Kijana wake tangu mwaka 2011 na baada ya kuhangaika kupata matibabu kwenye Hospitali kadhaa hapa nchini bila mafanikio na kutokana na hali ngumu ya kifedha waliamua kumuomba Mhe Rais msaada wa matibabu.

"Naendelea kumshukuru sana Mhe Rais Samia Suluhu Hassan na kumuombea katika uongozi wake kwa msaada huu wa matibabu aliotupatia, leo naona hali ya Kijana wangu inaendelea vizuri tofauti na alipoletwa Hospitali siku ya kwanza" alishukuru Bi. Aziza.

Aliongeza kuupongeza uongozi wa BMH na Wataalamu wake wote kwa kufanikiwa kumuondoa uvimbe huo kijana wake na kuongeza kuwa ameshatembea kwenye Hospitali nyingi lakini hakuwahi kufanikiwa kumaliza changamoto hiyo ya Kijana wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof Abel Makubi amesema kuwa mara baada ya Uongozi wa Mkoa wa Manyara kupata taarifa ya Kijana huyo kuomba msaada wa matibabu kwa Mhe Rais, kwa kushirikiana na idara ya Afya ya Mkoa huo waliweza kumleta Hospitali ya Benjamin Mkapa tarehe 25 Disemba, 2024 usiku ambapo alianza vipimo na asubuhi ya siku iliyofuatia kijana huyo akafanyiwa upasuaji wa kuondolewa uvimbe huo.

"Kwa sasa Kijana Hussein yuko wodini akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea kuimarika, Nimshukuru sana Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji Mkubwa kwenye Sekta ya Afya na BMH na kuwezesha wananchi hata wasio na uwezo wa kifedha kupata matibabu kwa magonjwa yanayo wasumbua" amesisitiza Prof Makubi.

Akielezea hali yake Kijana Hussein Idd Babu (18) ameshukuru kwa huduma ya matibabu aliyopewa na kusema anaona anaendelea vizuri na ameahidi akipona ataendelea na majukumu yake ikiwemo kurudi shule kuendelea na masomo ya elimu ya msingi ambayo aliyakatisha kutokana na tatizo hili lililomsumbua kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment