Na Okuly Julius, Dodoma
Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Taasisi yake ya Watumishi Housing Investments (WHI) imeandaa hafla muhimu ya Uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma utakaozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango Disemba 11, 2024 katika eneo la Mradi wa Nyumba Njedengwa, jijini Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo Disemba 04, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi yake iliyopo kwenye jengo la Mkapa Jijini Dodoma.
“Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, inapenda kuwaalika Watanzania wote kushiriki katika hafla hii muhimu ambayo inaashiria hatua kubwa katika kuboresha maisha ya Watumishi wa Umma na maendeleo ya sekta ya makazi Nchini.” Mhe. Senyamule
Aidha, Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji Sera – Ofisi ya Rais Utumishi Dkt. Fred Msemwa amesema;
“Siku hiyo utazinduliwa mpango wa Mradi wenye nyumba 206 ambazo zimeshajengwa ambapo nyumba zaidi ya 200 tayari zinatumika pia mahitaji ya nyumba za watumishi ni zaidi ya 200,000 hivyo, kinachofanyika sasa, mpango unalenga kuweka mkakati wa kujenga nyumba nyingi zaidi nchi nzima ili kukabiliana na upungufu wa makazi unaowakabili Watumishi wa Umma.” Dkt Msemwa.
Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ulianza kutekelezwa mwaka 2014 chini ya usimamizi wa WHI na hadi sasa zaidi ya nyumba 1000 zimejengwa katika mikoa 19 nchini ikiwemo Dodoma, Dar Es Salaam, Mwanza, Morogoro, Simiyu, na Mtwara ambapo unalenga kuwawezesha wananchi na hasa Watumishi wa Umma kiuchumi kupitia umiliki wa nyumba.
No comments:
Post a Comment