ACHEPUSHA MAJI NA KUTUMIA KATIKA KILIMO CHA BANGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 18, 2025

ACHEPUSHA MAJI NA KUTUMIA KATIKA KILIMO CHA BANGI



Na Mwandishi Wetu _DODOMA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) katika Operesheni ya ukusanyaji wa Madeni kwa wateja wenye Madeni Sugu na ukaguzi wa Miundombinu imebaini uwepo wa Mteja aliyechepusha maji (kuiba Maji) na kutumia katika kilimo cha zao haramu la Bangi.

Akizungumza mara baada ya Operesheni ya leo iliyofanyika katika Mtaa wa Hamvu, Kata ya Chang'ombe, Meneja Ankara na Udhibiti wa Madeni DUWASA GEORGE MWAKAMELE amesema hatua hiyo inakuja baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria Wema.

"Tulipata taarifa za siri juu ya mteja wetu huyu ,na tulianza kumfatilia na kubaini kuwa amekuwa akitumia maji yetu katika kilimo hasa Bangi na shughuli zake amekuwa akifanya ndani ya eneo hili ambalo amejifungia ndani ya uzio huu mkubwa " ameeleza Meneja Ankara na Udhibiti wa madeni kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma DUWASA Mwakamele

Mwakamele ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa juu ya vitendo ama viashiria vyovyote vya uwepo wa matukio ya uharibifu wa miundombinu yam aji katika maeneo yote nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Hamvu HALID MAJID amesema kitendo alichokifanya Mwananchi huyo aliyemtaja kwa jina la Hood Rajabu la kuchepusha maji isivyo halali imesababisha baadhi ya maeneo ya mtaa huo kuwa na upungufu wa maji.

"Vitu kama hizi wasifanye wafuate taratibu za kisheria,Duwasa wanautaratibu wa kulipa madeni kidogo kidogo,hakuna sababu ya kuiba maji na Mbaya zaidi maji hayo unatumia kulima dawa za kulevya na kuvunja sheria katika eneo letu"

Na kuongeza kuwa "ukiangalia eneo hili ameweka uzio mrefu wa ukuta na hakuna mtu anaweza kuingia ndani wala kujua kinachoendelea kama kuna kilimo cha bangi lakini amekuwa akichangua nani wa kuingia ndani "Mwenyekiti wa mtaa wa Hamvu HALID MAJID

Amesema awali Hood Rajabu alikuwa ni Mwananchi mwenye utii wa sheria lakini baadae alibadilika na kuanza kutumia madawa ya kulevya .

Amesema baada ya kugundua jambo hilo wamewataarifu majirani kuwapa taarifa kwa maeneo mengine yenye vitendo vya kuvunja sheria

Mtendaji wa Mtaa huo MARIAM KASELEKO ameeleza kusikitishwa kwa tukio hilo na kuahidi kuanza kufanya ufuatiliaji wa maeneo ambayo hayajaendelezwa.

"wito wangu tu kwa wananchi ni kutoa ushirikiano hasa katika maeneo ambayo wataona kuna viashiria kama hivi ila kuweza kutokomeza matukio haya na hili linatuhamasisha kufanya ufuatiliaji wa maeneo ambayo hayajaendelezwa ili kubaini nini kipo ndani yake," ameeleza KASELEKO

Ibrahim Mafita ni mkazi wa kata ya Chang'ombe amewasii wananchi wenzake kufuata utaratibu pindi wakiwa na madeni ili kujiepusha na uchepushaji wa maji.

"Suala la matumizi ya maji kinyume cha kisheria ni jambo ambalo halikubaliki alafu zaidi unatumia kulima kilimo haramu sio jambo jema ,ni muhimu wananchi tutumie utaratibu wa kisheria wa kulipa madeni ambao umewekwa na DUWASA"

Kwa mujibu wa taarifa ,Mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi huku Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma ikiendelea na kampeni ya usitishaji wa huduma ya maji kwa wateja ambao ni wadaiwa sugu.



No comments:

Post a Comment