OR-TAMISEMI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, imeielekeza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhakikisha Halmashauri zote nchini zenye mapato makubwa ya ndani zinajenga uzio katika maeneo ya kutolea huduma za afya kwa ajili ya usalama wa wananchi na mali za umma.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justin Nyamoga ametoa maelekezo hayo wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya elimu na afya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
“Tukipita kwenye maeneo mengi tunaona hospitali hazina uzio. Kutokana na maeneo mengi kuwa karibu na makazi ya watu, Kamati inashauri Halmashauri zenye mapato ya ndani ya kutosha zianze kujenga uzio kwenye maeneo ya huduma za jamii kama haya,” amesema Mhe. Nyamoga.
Ameongeza kuwa ni muhimu maeneo yanayotoa huduma za afya kuwa salama na kuhakikisha faragha kwa wagonjwa na wateja wanaoingia na kutoka.
Pamoja na hilo, Mhe. Nyamoga amezitaka Halmashauri zote nchini kufuata miongozo na taratibu katika matumizi ya fedha za miradi ya BOOST na SEQUIP, ili Watanzania waendelee kunufaika na juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, amepokea maelekezo hayo huku akisisitiza umuhimu wa Halmashauri kuendeleza miundombinu katika sekta nyeti, ikiwamo sekta ya afya.
Kamati hiyo imemaliza ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Pwani, ambapo imetembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji wa Rufiji na Manispaa ya Kibaha.
No comments:
Post a Comment