
Na Okuly Julius _DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Kimataifa wa Msalato pamoja na ujenzi wa Barabara ya Mzunguko nje ya Dodoma (outer Ring Road) inayoendelea jijini Dodoma.
Akizungumza wakati kamati hiyo ilivyotembelea kukagua na kuona maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso amesema mpaka hatua hiyo iliyofikiwa miradi hiyo inakwenda vizuri na Tayari thamani ya fedha inayotolewa na Serikali imeanza kuonekana.
Kuhusu Uwanja wa Kimataifa wa Msalato Kakoso ameshauri kuwepo na eneo maalumu kwa ajili ya kusafirisha mazao mbalimbali kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi ili kuongeza uchumi wa wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
" Sisi kama Kamati tumeridhishwa Sana na kasi ya ujenzi wa uwanja huu ila kamati inashauri ujenzi wa eneo la kuhifadhi mazao kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi,, mfano mbogamboga na matunda,, ikumbukwe kuwa hapa Dodoma kunalimwa zabibu hivyo tukitengeneza mazingira mazuri ya kusafirisha basi Uwanja huu utakuwa na manufaa makubwa, "ameeleza Kakoso
Katika hatua nyingine Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi, kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), kuhakikisha ulinzi wa Eneo la Uwanja unakuwepo ili kuepukana na wanachi kuvamia maeneo hayo na kusababisha migogoro wakati wa kuwatoa na kupelekea Serikali kuanza kulipa fidia.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa Uwanja huo umezingatia viwango vyote vya Kimataifa na kuihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara ya Ujenzi imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na yatatekelezwa.
Kuhusu Barabara ya Mzunguko Kakoso amepongeza uwekaji wa vivuko visivyoingiliana na barabara hiyo pamoja na ujenzi wa madaraja kwenye maeneo korofi, huku akisisitiza barabara hiyo izingatie ubora na kusiwepo na matuta mengi ya kupunguza mwendo ili kufanya barabara hiyo kuwa na upekee wake.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 112.3 ambao ndio mzunguko mzima wa Mji wa Dodoma na barabara hii imezingatia watembea kwa miguu kila upande ina mita 2.5 za watembea kwa miguu.
"barabara hii ni kielelezo kwa miradi ya Kimkakati inayoendelea hapa nchini kwani imezingatia mahitaji ya sasa ya Jiji la Dodoma na kukamilika kwake itaondoa msongamano katikati ya jiji kwani malori hayataoneoana tena mjini, " ameeleza Kasekenya

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amesema kuhusu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ndege zinatarajiwa kuanza kutua kuanzia Julai na kuendelea kwani yale maeneo muhimu kwa ajili ya ndege kutua yatakuwa yamekamilika.



No comments:
Post a Comment