OR-TAMISEMI
Ofisi ya Rais-TAMISEMI imezielekeza ofisi za wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha kuwa rasimu za mikataba ya huduma kwa mteja zinawasilishwa ifikapo Februari 20, 2025.
Rasimu hizo zitafanyiwa maboresho kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa ajili ya idhini ya matumizi rasmi, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Miundo, Peter Mhimba ameyasema hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, alipokuwa akifunga mafunzo ya uandaaji wa mikataba ya huduma kwa mteja kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Utawala na Rasilimaliwatu pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kutoka ofisi za wakuu wa mikoa yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.
"Tunahitaji kuona rasimu hizi zikifikishwa TAMISEMI kwa wakati ili zifanyiwe maboresho kabla ya kuwasilishwa kwa UTUMISHI ifikapo Machi 31, 2025 kwa ajili ya idhini rasmi," amesisitiza Mhimba.
Aidha, amewasihi viongozi wa sekretarieti za mikoa kuhakikisha mikataba hiyo haikai kwenye makabati mara tu inapokamilika, bali izinduliwe rasmi na kuwafahamisha wananchi kuhusu umuhimu wake katika kuboresha huduma za serikali.
Kwa niaba ya Makatibu Tawala, Emmanuel Kayuni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya, ameahidi kutekeleza maelekezo hayo kwa wakati na kuhakikisha mikataba inawasilishwa kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Khadija Dalasia, ameahidi kuwa watahakikisha wananchi na wadau wote wanapata taarifa kuhusu mkataba huo kupitia tovuti, mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, na nakala zilizochapishwa.
Mafunzo hayo ya siku nne yameendeshwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa lengo la kuhakikisha kila mkoa unaandaa na kutekeleza mkataba wa huduma kwa mteja kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment