Na. Eva Ngowi -WF -Dar es Salaam
Wizara ya Fedha kupitia Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – PPP, imeziasa Wizara na Taasisi zilizoshiriki kikao kazi cha kupitia marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP), pamoja na kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Sera ya Taifa ya PPP ya miaka mitano (2021/22 – 2025/26), kuwa wabunifu wakati wa kuandaa miradi ya PPP.
Hayo yameelezwa na Kaimu Kamishna wa Kitengo cha PPP, Wizara ya Fedha, Bw. Bashiru Taratibu wakati akitoa wasilisho kwa Wizara na Taasisi kuhusiana na Utekelezaji wa Mkakati wa Sera ya Taifa ya PPP ya Miaka Mitano, katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dar es Salam.
Bw. Taratibu alisema kuwa ubunifu ukitumika katika utekelezaji wa majukumu waliyonayo utasaidia kupata vyanzo mbadala vya rasilimali fedha na kupunguza muda wa kusubiri fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi maendeleo.
“Kila Taasisi imepewa majukumu mahsusi, yanayotakiwa kufanywa kwa kutumia “resource” (rasilimali)zinazotoka Serikalini, unaweza ukajikuta rating yako kila mwaka inakuwa kwenye kiwango cha chini kwa kuwa unakuwa hupati rasilimali fedha za kutosha na kwa wakati. Kwa hiyo tuwe wabunifu ili kuhakikisha tunapeleka huduma nzuri kwa jamii.” Alifafanua Bw. Taratibu.
Aidha, kikao kazi hicho kilijadili mada mbalimbali zikiwemo; Dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi -PPP, Utekelezaji wa Mkakati wa Sera ya Taifa ya PPP (2021/22-2025/26), Marekebisho ya Sheria ya PPP, Sura 103 na Kanuni za PPP 2023, Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma, Waraka Na.5 na 7 wa Hazina wa Mwaka 2021.
Kikao kazi hicho cha siku sita, kimeshirikisha baadhi ya Wizara na Taasisi zikiwemo Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi na Tume ya Taifa ya Mipango. Taasisi zilizoshiriki ni Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka- DART, Shirika la Maendeleo na Uchumi la Jiji la Dar es Salaam- DDC, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili - MOI, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania – TAA, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania – GBT, Wakala wa Majengo Tanzania – TBA na Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA.
No comments:
Post a Comment