DARAJA LA NYANTARE KUWAUNGANISHA WANANCHI VIJIJI VYA NYANTARE NA MTUMBA, KASULU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 19, 2025

DARAJA LA NYANTARE KUWAUNGANISHA WANANCHI VIJIJI VYA NYANTARE NA MTUMBA, KASULU



Kasulu, Kigoma


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara inaendelea na ujenzi wa daraja la mawe la Nyantare lenye urefu wa mita 32 pamoja na kufungua barabara ya Mirambo Km 2 ili kuunganisha Kijiji cha Nyantare na mtaa wa Mtumba katika kata ya Nyasha halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma.

Mhandisi wa TARURA wilaya ya Kasulu ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo, Hayaishi Ruige amesema kuwa mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 90 umelenga kuwasaidia wananchi waweze kufikia huduma za kijamii ikiwemo shule na zahanati kwa urahisi.

“Awali wananchi walikuwa wanazunguka Km 10 kwenda upande wa pili ambao kuna shule na zahanati lakini sasa watatumia Km 2 tu kuzifikia huduma hizo ambapo barabara itajengwa kwa kiwango cha changarawe”, amesema.

Naye, Mhe. Patrick Kazuzuru Diwani wa Kata ya Nyasha amesema kuwa, ujenzi wa daraja la Nyantare ni mkombozi kwa wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi zinazopatikana ng’ambo ya pili kama vile zahanati, shule ya msingi na sekondari ambapo awali walikuwa wanapata shida kuvuka kuzifikia huduma hizo, hivyo wanaishukuru serikali.

Bi. Ester Hussein mkazi wa Nyantare ameipongeza serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo awali mvua ikinyesha walikuwa wakisubiri masaa 3 hadi 4 mpaka mvua iishe ili kuwavusha watoto wao kwenda shuleni, lakini sasa wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hilo.

Naye, mkazi wa Nyantare, Bw. Essau Elias ameeleza kuwa mto huo Mgandazi umewatesa zaidi ya miaka 30, awali kipindi cha masika walikuwa hawawezi kuvuka kwenda Mtumba ambapo kuna zahanati kuwapeleka wake zao kwenda kujifungua lakini sasa wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja hili ambapo wanafika zahanati bila shida yoyote.




No comments:

Post a Comment