KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) imesema kukamilika kwa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kutapunguza malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi kuhusu kupunjwa kwenye vipimo vya bidhaa zao.
Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Augustine Vuma, ameyasema hayo leo Machi 13, 2025, wakati wa ziara ya kamati hiyo kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya WMA Makao Makuu, ambapo pia kutakuwa na ofisi za mkoa wa Dodoma.
Alisema kuwa mradi huo wa bilioni sita utasaidia kutatua changamoto na malalamiko mbalimbali ya wafanyabiashara na wananchi kuhusu vipimo, kwani ofisi hizo zitakuwa na maabara za kisasa za vipimo.
"Watanzania wamekuwa na changamoto na malalamiko mengi kuhusu kupunjwa kwenye manunuzi mbalimbali, ikiwemo vinywaji na vyakula viwandani na majumbani," amesema.
Aidha, alisema kuwa mradi huo utachangia uwepo wa mazingira mazuri ya kufanyia kazi, kuhamasisha ubunifu zaidi na kuongeza tija.
Ameeleza kuwa kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo uliotekelezwa na kampuni ya wazawa, jambo linaloonyesha kuwa wakandarasi wa ndani wanaweza kutekeleza kazi nzuri na bora.
"Usimamizi mzuri umefanyika, na kwa vile mradi umetekelezwa na wakandarasi wa ndani, fedha zimebaki hapa nchini," amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah, alisema kuwa ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Wakala ulikabidhiwa rasmi Machi 10, 2025.
"Tunahitaji kuona Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PIC imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu kwa asilimia 100. Mradi umekamilika kwa wakati, na kamati imetoa mapendekezo kipindi cha uangalizi ili dosari zozote zitakazojitokeza ziweze kurekebishwa," alisema.
Alisema kuwa jengo hilo litatumiwa na watumishi wa makao makuu pamoja na ofisi za mkoa wa Dodoma.
"Tayari jengo limekabidhiwa, na kadri iwezekanavyo, watumishi watahamia Dodoma," aliongeza.
Aidha, alisema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawawezesha wafanyakazi wa wakala kuongeza ari na utendaji kazi kutokana na kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Pia kutakuwa na mazingira bora ya kuhifadhi vifaa vya kitaalam, hivyo kukidhi matakwa ya Shirika la Vipimo Duniani (OIML).
"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kiuchumi yaliyoiwezesha wakala kugharamia utekelezaji wa mradi huu kwa fedha za serikali," alisema.
Naye, Mshauri Elekezi kutoka MUST Consultancy Bureau Limited, Blasius Venance, alisema kuwa wamepokea maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya PIC kuhakikisha kuwa jengo halina dosari hata moja.
No comments:
Post a Comment