
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe George Simbachawene (wa pili kutoka kulia) akizindua makubaliano ya ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Hafla iliyofanyika leo Machi 6,2025 jijini Dodoma.
Na Okuly Julius _DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe George Simbachawene amesema kuzinduliwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) unakwenda kuleta mwamko kwa watu wengi kufahamu na kuelewa suala la maadili na Utawala Bora wakiwa bado hawajashika nafasi za uongozi wa Umma.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Machi 6,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Makubaliano hayo.
Amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha kwa kuona umuhimu wa kuingia makubaliano na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwani ni njia sahihi ya kuzalisha watu wenye maadili hata kabla hawajashika nafasi za uongozi katika taasisi za umma au sekta binafsi.
Waziri Simbachawene amesema kuwa ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kwa kuhakikisha kuwa elimu ya maadili na utawala bora inakuwa sehemu ya mifumo ya kitaasisi na kitaaluma nchini, Vyuo na taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuendelea kushirikiana na serikali ili kuimarisha mitaala inayohusiana na uadilifu, uwajibikaji, na utawala bora.
"pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali, bado tunakabiliana na changamoto za ukiukwaji wa maadili katika sekta mbalimbali. Changamoto hizi ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, mgongano wa maslahi, na ufujaji wa rasilimali za umma,"
Na kuongeza "Uadilifu katika uongozi wa umma ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa letu. Viongozi wote na watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano bora wa uwajibikaji, uaminifu, na utendaji wa haki. Taifa lenye viongozi waadilifu linakuwa na taasisi imara, zenye kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa maadili ya utumishi wa umma yanazingatiwa ili kujenga imani kwa wananchi na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma," ameeleza Simbachawene

Kamishina wa Maadili Mhe. Jaji (Mst) Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi. amesema Mafunzo yatakayotelewa kupitia makubaliano hayo yatawasaidia kuwaelimisha viongozi wa Umma kuhusu umuhimu wa kuepuka mianya ya Rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Hivyo, amewataka washiriki wa Makubaliano hayo kila mmoja kuhakikisha anakuwa Balozi wa maadili na kuhamasisha Utamaduni wa uwajibikaji na uadilifu ndani ya Taasisi aliyemo na kwingineko.
" Tanzania yenye maadili Imara ni Tanzania yenye maendeleo Endelevu hivyo kupitia ushirikiano huu ambao umeanzishwa leo kati ya Chuo cha Uhasibu Arusha na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ninaamini tunaweza kujenga mfumo Imara wa maadili unaozingatia misingi ya haki, usawa na Utawala Bora, "ameeleza Jaji Mstaafu Mwangesi

Mwenyekiti wa Bodi ya IAA Dkt. Mwamini Madhehebi Tulli amesema mafunzo hayo mbali tu na kuwasaidia viongozi wa Umma waliopo kwa sasa pia itawasaidia viongozi wa Umma wanaokuja kwani watakuwa wamepata mafunzo ya Maadili tangu wakiwa Vyuoni na kuomba ushirikiano huo usiishie tu IAA uende katika vyuo vingine ila kusaidia Taifa kuzalisha vijana wenye maadili.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka amesema Chuo hicho sio tu kinawajibika kutoa mafunzo katika sekta mbalimbali za uchumi bali Vilevile katika maadili ya watumishi wa umma
Amesema Chuo hicho kinaendelea kutoa programu mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya sasa na inayotegemewa katika Umma na kinahakikisha kwamba kinatoa katika weledi na maadili ya hali ya juu.
"katika program hizi tunakusudia kuwajengea ujuzi wataalam mbalimbali katika kutumia mifumo ya kidijitali kuimarisha maadili katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha uongozi wenye uwajibikaji katika taasisi zote,"
Na kuongeza"sisi IAA tunaamini kuwa elimu bora ni mwelekeo wa Teknolojia na maadili ni msingi wa ufanisi katika Utawala Bora wa Taifa letu, "amesema Prof. Sedoyeka
Amesema chuo hicho kinaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi na sasa wanakwenda kushirikiana na Tume ya Maadili na hiyo inawasaidia kama Chuo kuangalia maeneo mapana ya muktadha wa maendeleo ya taifa na sio kutoa elimu tu.

Awali akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Natu El-maamry Mwamba, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Fedha Simbani Liganga, ametoa pongezi kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha kwa kusukuma mbele agenda ya Maadili na uwajibikaji na inatekelezwa kwa vitendo kwani itasaidia kuongeza uwajibikaji, uwazi na haki katika maeneo ya kazi hasa Utumishi wa Umma.







MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA HAFLA YA UZINDUZI WA MAKUBALIANO NA USHIRIKIANO KATI YA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA NA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA (IAA), HAFLA ILIYOFANYIKA LEO MACHI 6,2025 JIJINI DODOMA.
No comments:
Post a Comment