
Na Mwandishi Wetu.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi Habari Tanzania (JAB) imepanga kutoa kadi za kidijitali ili kulinda wanahabari katika suala la utunzaji wa taarifa zao.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 18 Machi, 2025 jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Bodi hiyo, Mgaya Kingoba, wakati akijibu maswali wakati wa mahojiano na Mtangazaji wa Crown Media Salim Kikeke kuhusu bodi hiyo na jinsi ilivyojipanga kuwahudumia wanahabari ikiwa ni pamoja na kuwathibitisha na kuwapa Vitambulisho vya Kidijitali.
Bw. Kingoba amesema JAB imejipanga kufanya kila jambo kisasa ili kuwapunguzia adha waandishi ya kubadilisha vitambulisho kila mwaka.
Amesema vitambulisho vipya vinalenga kumpa heshima Mwandishi, kutambua taaluma yake na kumrahisishia kwani vitaunganishwa na mifumo mingine ya kidijitali nchini na kwamba gharama yake ni shilingi 50,000/= na kitatumika kwa miaka miwili.
Ameongeza kuwa masharti ya upatikanaji wa kitambulisho itakuwa ni elimu ya kuanzia ngazi ya Stashahada (Diploma) au Shahada (Degree) ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma.
Alipoulizwa kuhusu wakongwe ambao wamekuwa wakifanya kazi ya uandishi wa habari kwenye vyumba vya Habari bila kuwa na hata taaluma ya uandishi wa habari ya Kiwango cha chini cha Stashahada, Bw. Kingoba amesema Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake imewataja watu kama hao na watazingatiwa kwani wanatambulika kwa mchango wao mkubwa kwenye tasnia ya habari.
No comments:
Post a Comment