Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, jijini Dodoma. |
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan , biashara ya mbolea nchini imekua, ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya hiyo, Bw. Joel Laurent wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 19, 2025, jijini Dodoma.
Aidha, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024, uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.
"Kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji nchini pamoja na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeshuduia kuongezeka kwa viwanda vya kuzalisha mbolea na visaidizi vya mbolea kutoka viwanda 16 mwaka 2020/2021 hadi viwanda 33 mwaka 2023/2024. Kati ya viwanda hivyo, vitatu (3) ni vikubwa, viwanda 11 ni vya kati na viwanda 19 ni vidogo, "ameeleza Bw.Laurent
Bw. Laurent amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, taifa limeshuhudia ongezeko la matumizi ya mbolea kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024.
Aidha, Ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.
"Lengo ni kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta ifikapo mwaka 2033 kwa kuzingatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi za Afrika yaliyofanyika Nairobi 2024,"
Na kuongeza kuwa "kuongezeka kwa matumizi ya mbolea nchini kumechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 19,980,718 mwaka 2020/2021 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 14 na kufanya utoshelevu wa chakula nchini kufikia asilimia 128, "amesema Mkurugenzi huyo
Katika hatua nyingine Bw. Laurent amesema TFRA imeimarisha matumizi ya TEHAMA ambayo yamepunguza muda na gharama za kupata huduma kwa wateja hasa muda wa kupata leseni na vibali vya kuingiza na kusafirisha mbolea nje ya nchi umepungua kutoa siku 14 hadi siku mbili (2).
Vilevile, matumizi ya mifumo yamewezesha upatikanaji wa takwimu za uhakika zinazoiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza tasnia ya mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.
"kupitia Mfumo wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System), wakulima wanaendelea kupata fursa ya kuingizwa kwenye mifumo rasmi ya kifedha kupitia Kadi Janja na fursa ya kupata Hati Miliki za mashamba, uwezeshaji wa huduma za kibenki pamoja na huduma nyigine muhimu,"ameeleza Bw. Laurent
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni Taasisi iliyo chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 9 ya Mwaka 2009 kwa lengo la kusimamia tasnia ya mbolea kwa kudhibiti ubora na biashara ya mbolea nchini.
No comments:
Post a Comment