
Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA - MACHI 19, 2025
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanikiwa kufanya operesheni ya kwanza ya ubongo kwa kutumia Teknoljia ya Mawimbi ya Sauti na kufanikiwa kutoa damu yote iliyokuwa imevia kwenye ubongo wa mgonjwa.
Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano cha BMH Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ambaye ndio aliongoza Jopo la Madaktari waliofanya Upasuaji huo wa kutumia Teknolojia ya Mawimbi ya Sauti Dkt. Maxigama Ndosi amesema kuwa wamefanikiwa kutibu mvilio wa damu kwenye ubongo wa Mgonjwa kwa kusaidiwa na Mawimbi ya Sauti na kuitoa damu yote iliyovia kwenye ubongo.
"Hospitali ya Benjamini Mkapa imeanza kwa mara ya kwanza, matumizi ya Mawimbi ya Sauti kwa upasuaji wa kutoa damu na uvimbe kwenye ubongo (High-intensity Focused Ultrasound -HIFU), teknolojia hii inasaidia kufungua sehemu ndogo ya kichwa na kumuacha Mgonjwa na kovu dogo ambalo linapona kwa haraka" alibainisha Dr. Max.
Aliongeza kuwa utaalam wa kutumia mawimbi ya sauti utasaidia sana kupunguza muda wa upasuaji kwa Wagonjwa ambao wana damu kichwani na hata Wagonjwa wenye uvimbe ndani ya ubongo.
"Teknolojia hii (intraoperative Ultrasound neuronavigation) inasaidia katika upasuaji wa ubongo uwe wa kuondoa damu iliyovia kwenye ubongo kichwani au uvimbe kwa ajili ya saratani au wa namna nyingine na pia inaongeza ufanisi katika kufanya upasuaji wa aiana yoyote ya ugonjwa ndani ya kichwa" alifafanua Dr Max.
Aliongeza kuwa Teknologia hii ni ya kipekee hivyo BMH itaanza kufanya upasuaji kwa njia hii ili kuongeza ufanisi wa kupasua kuondoa damu ndani ya ubongo au aina nyingine ya saratani ndani ya ubongo.
"Maana yake tunaweza kusema mtu yeyote anayekuja hapa BMH mwenye changamoto kama hiyo na ujuzi huu tulionao (Teknolojia ya kutumia mawimbi ya sauti wakati wa upasuaji wa ubongo) utakaotumika kumtibu, miaka yote sisi BMH tutakuwa mbele katika kufanya operesheni hizi kwa ufanisi zaidi" aliahidi Dkt. Max.
Alimalizia kwa kumshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha BMH vifaa tiba na Wataalamu na kusema imesaidia kuboresha huduma za Afya kwa Watanzania wote na wageni kutoka nje ya Tanzania.
Nae Dkt. Kelvin Noel kutoka Idara ya Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu hapo BMH, amesema kuwa baada ya kumpokea Mgonjwa, walimfanyia vipimo na kubaini kuwa mbali na kupata tatizo la kiharusi (Stroke) Damu ilikuwa imevia kwenye ubongo wake hali ambayo ingehatarisha uhai wa Mgonjwa endapo asingepata matibabu muafaka na kwa wakati muafaka, hivyo jopo la Madaktari lilijadiliana na kuamua kumfanyia upasuaji wa Teknolojia hiyo ya Mawimbi ya Sauti na kufanikiwa kutoa Damu yenye ujazo wa Mililita 120 iliyokuwa imevia kwenye ubongo wa Mgonjwa.
Kwa upande wake Issa Kassimu ambaye ni Ndugu wa Mgonjwa aliyefanyiwa Operesheni hiyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za kisasa za Afya, vifaa tiba na Wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma za kibingwa; Aidha, aliishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa matibabu yote ambayo Mgonjwa wao ameyapata.


No comments:
Post a Comment