
Mahakama ya Tanzania imekabidhi makasha 10 ya kisasa ya Mahakama Mtandao kwa Jeshi la Magereza, yatakayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ili kusaidia utoaji haki kwa wakati, kupunguza msongamano wa wahalifu magerezani pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji wa wafungwa na mahabusu kwenda mahakamani kusikiliza mashauri yao.
Makabidhiano hayo yamefanywa kati ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, na Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP Jeremiah Y. Katungu, na kushuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, katika Gereza la Isanga - Dodoma, leo tarehe 21 Machi 2025.
Akizungumza baada ya kuzindua na kushuhudia makabidhiano hayo, Waziri Bashungwa amesema makasha hayo yatakayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ambao ni daraja linalounganisha mahabusu na haki na yatasaidia kupunguza gharama za usafiri pamoja na kuahirishwa kwa kesi kutokana na mahabusu kushindwa kufikishwa mahakamani.
"Mahakama Mtandao inarahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama, kuokoa gharama za uendeshaji, kupunguza msongamano wa wananchi mahakamani, kuwezesha mawakili kupata rejea za hukumu na nyaraka mbalimbali kwa urahisi, na pia kuwabaini mawakili vishoka ambao wamekuwa wakiharibu mwenendo wa kesi mbalimbali," amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ni mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kusaidia taasisi za haki jinai na kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Aidha, Bashungwa amelitaka Jeshi la Magereza kusimamia matumizi sahihi ya makasha waliyokabidhiwa, kuwa wabunifu, na kuendeleza mashirikiano kati ya taasisi za haki jinai.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema Mahakama ya Tanzania imeendelea kuwekeza katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati na kwa urahisi kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Magereza, CGP Jeremiah Y. Katungu, amesema Jeshi la Magereza limepokea makasha kumi kutoka Mahakama ya Tanzania, ambayo yamewekwa katika Magereza ya Keko, Ukonga na Segerea mkoa wa Dar es Salaam, Uyui mkoa wa Tabora, Karanga Moshi, Kisongo mkoa wa Arusha, Ruanda mkoa wa Mbeya, Maweni mkoa wa Tanga, Butimba mkoa wa Mwanza na Isanga mkoa wa Dodoma.
CGP Katungu amesema Jeshi la Magereza, kwa kushirikiana na Mahakama, limekuwa likifanya jitihada za matumizi na uimarishaji wa huduma za Mahakama Mtandao magerezani.







No comments:
Post a Comment