Mazingira Mazuri ya Biashara Yaongeza Kasi Utoaji Vibali vya Kuingiza Kemikali - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 14, 2025

Mazingira Mazuri ya Biashara Yaongeza Kasi Utoaji Vibali vya Kuingiza Kemikali



Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fedelice Mafumiko, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa ofisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 14, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO


Uwepo wa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji uliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita, umeongeza kasi ya utoaji vibali vya uingizaji na usafirishaji wa kemikali nchini kutoka vibali 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi vibali 158,820 kufikia Desemba, 2024.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 14, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.

Amefafanua kuwa, Mamlaka hiyo imeweka mazingira mazuri ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hatarishi na zile zinazodhibitiwa chini ya mikataba ya kimataifa ili kulinda afya ya binadamu, mazingira na usalama wa nchi kwa kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali hizo.

“Pamoja na uwepo wa mazingira mazuri, kasi ya utoaji vibali imeongezeka kutokana na wadau kuongeza uelewa wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za kemikali pamoja na kuwajengea wadau uelewa wa matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA inayotumika katika uombaji wa usajili na vibali. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 294 ya vibali vilivyotolewa”, amesema Mafumiko.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, mamlaka imeendelea kuchangia uboreshaji wa mazingira ya biashara ya kemikali nchini hasa zile za kimkakati zinazotumika kwenye uchimbaji na uchenjuaji wa madini hapa nchini na nchi jirani ambapo kemikali aina ya Ammonium Nitrate imeongezeka kutoka tani 135,445 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 359,629.56 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 165.52.

Vile vile, kemikali ya Salfa imeongezeka kutoka tani 396,982 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 1,136,214.86 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 186.21 huku kemikali ya Sodium Cyanide imeongezeka kutoka tani 41,461 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi tani 53,055.9 kufikia Desemba, 2024 sawa na ongezeko la asilimia 27.97.

Ametaja sababu za kuongezeka kwa uingizaji wa kemikali hizo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Tanga kuwa ni maboresho ya miundombinu ya bandari pamoja na mahusiano mazuri yaliyowekwa na Serikali kati ya nchi na nchi jirani.

No comments:

Post a Comment