NDOTO ZA PAMELA ZATIMIA BAADA YA MIAKA SITA, AZINDUA KITABU CHAKE CHA KWANZA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 8, 2026

NDOTO ZA PAMELA ZATIMIA BAADA YA MIAKA SITA, AZINDUA KITABU CHAKE CHA KWANZA



Na Boniphace John, OKULY BLOG - Dodoma


Baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka sita akifuatilia ndoto yake ya kuwa mwandishi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Pamela Bazoro Jerome, amefanikiwa kuzindua kitabu chake cha kwanza kiitwacho “Si Wewe Tu, Bali Ni Uwezo Uliomo Ndani Yako” (Not You, But Your Potential), chenye lengo la kuwahamasisha vijana na jamii kwa ujumla kutambua uwezo wao wa ndani katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Uzinduzi wa kitabu hicho umefanyika katika Kanisa la EAGT Oster Bay Makulu, jijini Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini, wahadhiri wa vyuo vikuu pamoja na wanafunzi. Hafla hiyo ilitanguliwa na ibada maalumu ya shukrani.

Akizindua kitabu hicho, Afisa Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Ezekiel Ndulani, alisema kitabu hicho ni zaidi ya mkusanyiko wa maandishi kwani kinabeba ujumbe wenye uwezo wa kubadili fikra na mitazamo ya watu, hususan vijana.

“Hatuzindui kitabu tu, bali tunazindua fikra, matumaini, maono na ujumbe utakaogusa maisha ya watu wengi. Pamela ametumia kalamu yake kuelimisha jamii kuwa mafanikio ya mtu hayazuiliwi na mazingira, changamoto au historia yake, bali huathiriwa na kushindwa kutambua uwezo alionao,” alisema Ndulani.

Aliongeza kuwa jamii inahitaji vitabu vinavyojenga matumaini, vinavyohamasisha ubunifu na kuwapa vijana nguvu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la ajira.

Aidha, alimpongeza Pamela kwa hatua hiyo kubwa ya kutumia kipaji chake kuifikia jamii kupitia uandishi, akibainisha kuwa uandishi ni kazi inayohitaji uvumilivu, maarifa, maono na nidhamu kubwa.

Kwa upande wake, Pamela alisema mafanikio hayo ni matokeo ya ndoto aliyokuwa akiifuatilia kwa muda mrefu, akieleza kuwa kitabu chake kinalenga kuwasaidia wasomaji kuamini uwezo wao na kutokata tamaa wanapokumbana na changamoto.

“Ndoto yangu ya miaka zaidi ya sita leo imetimia. Ninaamini kitabu hiki kitawasaidia watu wengi kutambua kuwa changamoto si mwisho wa maisha, bali ni sehemu ya safari ya mafanikio,” alisema Pamela.

Aliongeza kuwa anatamani kuona kitabu hicho kikisambazwa ndani na nje ya Tanzania ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma kutoka Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi, Dkt. Michael Msabi, alimpongeza mwanafunzi huyo kwa ujasiri na ubunifu aliouonyesha akiwa bado chuoni.

Alisema kitabu hicho kina ujumbe unaohamasisha kumtumaini Mungu, kutokukata tamaa na kujiamini katika kufikia malengo ya maisha.

Dkt. Msabi pia aliwataka vijana kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo na mitaji kwa makundi maalumu, ili kujiendeleza kiuchumi na kufikia ndoto zao.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa vijana na jamii kwa ujumla, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza maarifa, kukuza ubunifu na kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao ya kila siku.













No comments:

Post a Comment