
Na Okuly Julius _ DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kasi, huku vipande mbalimbali vya reli hiyo vikiwa katika hatua tofauti za ujenzi.
Akizungumza leo Machi 22, 2025, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma, Kadogosa amesema kuwa hadi kufikia Februari 2025, ujenzi wa kipande cha tatu cha Makutupora – Tabora (Km 368) umekamilika kwa asilimia 14.53, kipande cha nne cha Tabora – Isaka (Km 165) kimefikia asilimia 6.61, na kipande cha tano cha Isaka – Mwanza (Km 341) kikiwa asilimia 63.10.

Kadogosa ameeleza kuwa ujenzi wa Reli ya SGR umefikia hatua nzuri na kwamba kukamilika kwake kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uchukuzi na uchumi wa nchi.
"Ujenzi wa reli hiyo si tu utaboresha usafiri wa abiria kwa kasi na ufanisi mkubwa, bali utaimarisha pia usafirishaji wa mizigo, kupunguza gharama za usafiri, na kuchochea maendeleo ya miji inayopitiwa na reli," amesema Kadogosa.
Pia, amebainisha kuwa Serikali kupitia TRC imeendelea kusaini mikataba mbalimbali ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kisasa ili kuhakikisha uendeshaji wa reli hiyo unakuwa wa kiwango cha kimataifa.
Amefafanua kuwa hadi kufikia Desemba 2024, vichwa vyote 17 vya treni za umeme vimewasili nchini, na seti 10 za treni za abiria za umeme zimepokelewa na kufanyiwa majaribio.
Aidha, ameeleza kuwa huduma za usafirishaji wa abiria kwa kutumia SGR kati ya Dar es Salaam na Makutopora zilianza rasmi Juni 2024, na hadi sasa zaidi ya abiria milioni 2.1 wameshasafirishwa, huku mapato yaliyokusanywa yakiwa shilingi bilioni 59.
Kadogosa amebainisha kuwa huduma za usafirishaji wa mizigo zinatarajiwa kuanza mwezi Aprili 2025 baada ya kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 ya mizigo.
Kadogosa amesema kuwa miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira, kupunguza gharama za matengenezo ya barabara kwa kuhamasisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli, na kuchangia ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
"Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na mfumo bora wa reli utakaosaidia kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi wake," alisisitiza.


No comments:
Post a Comment