WANANCHI WA BAHI KINTINKU WAONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAWASILIANO YA BARABARA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 22, 2025

WANANCHI WA BAHI KINTINKU WAONDOKANA NA CHANGAMOTO YA MAWASILIANO YA BARABARA.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.

Wananchi wa Bahi Kintinku mkoani Dodoma wameondokana na adha ya msongamano wa magari baada ya serikali kutengeneza daraja ambalo ni makutano kati ya barabara ya Dodoma na Singida pamoja na miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22, 2025 jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Wakala Ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mha. Mohamed Besta ametoa rai kwa watumiaji wa barabara hiyo kufuata kanuni, alama na maelekezo ya barabara ili kupunguza ajali na uharibifu wa miundombinu hiyo.


Amesema barabara hiyo ni muhimu kwani ndio njia kuu ya magari yanayotoka Dodoma kuelekea Singida pamoja na nchi za jirani.


“Eneo hili lilikuwa eneo ambalo ni moja kati ya maeneo ambayo yalitakiwa kufanyiwa kazi na juzi tarehe 19 tukishirikiana na wenzetu wa shirika la reli tumeweza kukamilisha ujenzi wa eneo hili ambalo lilikuwa linasababisha msongamano mkubwa kwa kuwa lilikuwa katika matengenezo ya ujenzi wa daraja ilireli pamoja na magari yaweze kupishana,”


“Nimeridhishwa kwa kazi walioifanya ya usimamizi ya wataalam wa ujenzi wa barabara za rami kutoka ofisi ya meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma na ni kazi nzuri kwa kumsimamia mkandarasi vizuri kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa halileti tena ile changamoto iliyotokea hapo mwanzo”. amesema Mha. Besta.


Sambamba na hayo Mha. Besta amesema TANROADS baada ya kukamilisha zoezi hilo imeelekea Mkonze kwa matengenezo ya barabara ya mapishano kati ya reli ya SGR na barabara iendayo Iringa.


Nae Mkuu wa kitengo cha matengenezo TANROADS Mkoa wa Dodoma Mha. Elisony Mweladzi amewataka madereva kutunza thamani ya barabara hiyo.


“Tuwasihi tu watumiaji wa barabara waweze kutunza thamani za barabara zetu, eneo hili limejengwa kwa gharama kubwa, tunawasihi sana hasa madereva wa magari makubwa, malori waweze kuendesha kwa kufuata alama za barabarani, kuzingatia mwendo lakini pia wasitupe takataka ovyo na kumwaga mafuta barabarani wanapotengeneza magari yao,” amesema Mha. Mweladzi.


Kwa upande wake Hassan Lugazo ambaye ni dereva (msafirishaji) kutoka kampuni ya Franco ameishikuru TANROADS kwa uboreshaji wa barabara hiyo kwani awali ilikuwa changamoto kwao kwa uharibifu wa vyombo vya moto kutokana na kuwa na mabonde kipindi cha mvua huku ikisababisha msongamano wa magari.


Nae afisa usafirishaji (bodaboda) Paulo Samuel amesema walikuwa wanapata shida wakati wa kupita kutokana na ubovu wa barabara hiyo iliyosababisha madereva wa magari makubwa kutowapa nafasi (kuwabana)  lakini kwa matengenezo hayo ya TANROADS yamekuwa msaada kwao.










No comments:

Post a Comment