Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuitunza na kuifanyia matengenezo Miradi yote ya Barabara iliyofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mradi wa Agri-Connect.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa sherehe za ufungaji rasmi wa Mradi huo baada ya kukamilika iliyofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Kusindika Mazao ya Matunda na Mboga mboga, Jijini Mbeya.
"Tunaishukuru sana Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ambao walitupa fedha za msaada kwa maana 'Grants' kiasi cha Euro milioni 100 sawa na shilingi bilioni 265 fedha za kitanzania ambazo zimetumika kwenye ujenzi wa barabara Km. 166" amefafanua.
Mhe. Silinde ameahidi kuwa Serikali kupitia TARURA itaendelea kuzitunza kwa kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara kila itakapobidi barabara zote zilizojengwa kupitia mradi huo wa Agri- connect kwa kuzitengea bajeti ili ziendelee kuleta tija zaidi kwa wananchi.
Naye, Mratibu wa Mradi wa Agri-Connect kutoka TARURA Mhandisi Claver Mwinuka amesema Miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa wananchi kwani itarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda kwenye maeneo ya masoko na viwanda ambavyo vimeandaliwa kwaajili ya kuyachakata mazao hayo ili kuyaongezea thamani zaidi.
Wakati huo huo Balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini Mhe. Christine Grau amefarijika na ahadi ya Serikali ya kuzitunza barabara hizo ili ziendelee kutoa huduma endelevu kwa wananchi waliopitiwa na miradi hiyo.
Hafla hiyo ilienda sambamba na uzinduzi wa barabara za Masebe-Bugoba-Lutete Km 7.2 na Mpunguso TTC-Bugoba Kibaoni Km. 5 zilizojengwa kwa kiwango cha lami wilayani Rungwe, mkoani Mbeya ikiwa ni sehemu ya Miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa inayofadhiliwa na jumuiya hiyo.
Mradi wa Agri-Connect unalenga kuongea mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo hususani chai na mazao mengine ya matunda na mboga mboga na umetekelezwa katika mikoa mitano ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Songwe na Njombe.
No comments:
Post a Comment