
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuimarisha taasisi za umma na kuhakikisha zinatumia rasilimali za serikali kwa ufanisi huku zikifuata taratibu zinazotakiwa.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/24 na taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Rais Samia amesema ukaguzi uliofanywa na CAG unaonesha mwelekeo chanya wa serikali katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unaimarika.

"Pamoja na mapungufu yaliyotajwa na CAG, kwa ujumla kumekuwa na kuongezeka kwa ufanisi katika matumizi ya rasilimali za serikali," amesema Rais Samia, akisisitiza kuwa juhudi zaidi zinaendelea kufanywa ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa manufaa ya taifa.
Aidha, amepongeza TAKUKURU kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA ndani ya ofisi za umma, hatua ambayo imesaidia kupunguza changamoto zilizokuwepo miaka ya nyuma.
Pia, ameeleza kufurahishwa na jitihada za taasisi hiyo katika kuwajengea wananchi uelewa kuhusu rushwa, hususan kwa vijana wa shule za msingi hadi vyuo vikuu.
"TAKUKURU inajenga uelewa wa mapambano dhidi ya rushwa kwa vijana wa shule za msingi hadi vyuo vikuu. Hilo ni jambo zuri kwani watoto wakianza kufundishwa katika umri mdogo, wanakua na utamaduni huo ambao wamekuzwa nao," aliongeza Rais Samia.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya ripoti ya CAG na taarifa ya TAKUKURU, ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji nchini.


No comments:
Post a Comment