
Na Okuly Julius, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 149.83 kwa kutoa huduma za kibobezi katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), badala ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne ndani ya Taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya,amesema MOI imehudumia wagonjwa 7,366 waliopatiwa huduma za kibingwa ambazo hapo awali zilihitaji rufaa nje ya nchi.
Amesema kuwa gharama za matibabu hayo ndani ya Tanzania zilifikia shilingi bilioni 68.45, ikilinganishwa na shilingi bilioni 218.28 ambazo zingetumika kama wagonjwa hawa wangepelekwa nje ya nchi.
"Hatua hii sio tu imeokoa gharama kubwa kwa serikali, bali pia imeleta faraja kwa wananchi kwa kuwa na huduma hizi ndani ya nchi. Tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya makubwa katika sekta ya afya."
Amesema MOI imeendelea kuimarisha huduma zake kwa kuanzisha huduma mpya zaidi ya 10, kupanua miundombinu, kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha maslahi ya watumishi wake.
"Huduma mpya zaidi ya 10 zimeanzishwa, ikiwemo upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu, matibabu ya kiharusi kwa njia ya mishipa mikubwa ya damu, na kupandikiza viungo bandia kwa teknolojia ya ‘3D’," ameeleza Dkt. Mpoki
Pia amesema kuwa MOI imehudumia wagonjwa 816,383 katika huduma za nje na dharura, huku wagonjwa wa upasuaji wakifikia 30,289.
Ununuzi wa MRI na CT Scan mpya, vitanda vya kisasa, na ujenzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) lenye thamani ya Tsh. bilioni 10.8.
MOI pia imepeleka huduma zake katika mikoa mbalimbali, ikihudumia wagonjwa 44,096 na kufanya upasuaji kwa 5,382.
MIPANGO YA BAADAYE
MOI imepanga kuanzisha huduma mpya kama Banki ya Mifupa , matibabu ya Parkinson’s Disease, na ujenzi wa hospitali mpya ya utengamao Mbweni, Dar es Salaam.
Pamoja na hatua hizi, taasisi hiyo pia imeendelea kushirikiana na hospitali na vyuo vikuu vya kimataifa kwa ajili ya kubadilishana ujuzi na kufanya tafiti zitakazoboresha zaidi huduma za tiba nchini.
No comments:
Post a Comment