
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 20, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Okuly Julius _ DODOMA
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya uchukuzi kwa kuimarisha Chuo hicho kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 52.
Ambapo fedha hizo zimetumika kununua vifaa vya kufundishia na kuwajengea wakufunzi uwezo ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkuu wa Chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha chuo hicho kukamilisha maandalizi ya utoaji wa mafunzo ya urubani.
Amesema Mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza Mei 2025 baada ya chuo kukamilisha taratibu za kupata ithibati kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
"Kwa ajili ya mafunzo haya, Serikali imetoa takribani Shilingi Bilioni 6 ili kuwezesha utekelezaji wake," amesema Dkt. Mgaya
Dkt. Mgaya amebainisha kuwa hatua hiyo itapunguza gharama kwa asilimia 50-60 kwa watanzania waliokuwa wakisomea urubani nje ya nchi, na pia itaokoa fedha za kigeni.
Aidha, kuanzishwa kwa mafunzo hayo kutasaidia kuongeza idadi ya marubani wazawa na kupunguza utegemezi wa marubani wa kigeni ambao gharama zao ni kubwa.
Dkt. Mgaya amesema katika kuhakikisha Chuo kinaanza mafunzo ya Urubani Serikali imegharamia mafunzo ya wakufunzi watano (5),ambao wamepata mafunzo hayo nchini Afrika ya Kusini kwa Gharama ya TZS Bilioni 1.5 ikiwa ni wastani wa TZS Milioni 300 kwa kila mkufunzi.
Aidha Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo aina ya Cesna 172 zenye injini moja,ambazo tayari zipo nchini kwaajili ya kuanza mafunzo haya.
"Ndege hizi zina thamani TZS 2.9 Bilioni
Serikali ipo katika taratibu za ununuzi wa ndege nyingine tatu (3) ikiwa ndege moja ya injini mbili (2) ambayo itawasili mwezi Oktoba 2025 ambayo ina thamani ya TZS 5.9 Bilioni. Ndege mbili (2) za injini moja zitawasili mwaka 2026," ameeleza Dkt. Mgaya
Pia, serikali imetoa eneo lenye ukubwa wa Ekari 60 katika kiwanja cha KIA mahsusi kwaajili ya mafunzo haya ambapo ujenzi wa miundombinu unaendelea.
Aidha, katika kipindi cha miaka minne Serikali imegarimia mafunzo ya leseni kwa wakufunzi wa mafunzo ya uhandisi matengenezo ndege ambapo jumla ya wakufunzi nane (8) wamehitimu mafunzo ya leseni ya Uhandisi matengenezo ndege.
Wakufunzi wawili walisoma nchini Marekani na wakufunzi sita (6) nchini Ethiopia. Aidha, wakufunzi wawili bado wapo masomoni nchini Ethiopia katika Chuo cha Ethiopian Aviation Academy. Jumla ya TZS 1.2 Bilioni zimetumika kuwasomesha wakufunzi hao.
No comments:
Post a Comment