
Mkutano Maalumu wa 59 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umefanyika leo tarehe 5 Machi 2026 jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 7 Machi 2026.
Mkutano huo ambao umepokea na kujadili taarifa ya kikao cha Makatibu Wakuu, pamoja na masuala mengine umekamilisha maandalizi ya ajenda zitakazojadiliwa na kutolewa maamuzi pamoja na maelekezo na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC, ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi ndani ya Jumuiya hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Mhe. Beatrice Askul Moe Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Kenya na Mwenyekiti wa Mkutano huo ameeleza kuwa ajenda zilizoandaliwa zitatoa mwelekeo mpya wa utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya kwa sasa ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha za kuendesha shughuli mbalimbali za Sekretariati ya EAC na upungufu wa wafanyakazi.
Aidha, ametoa rai kwa wajumbe wa mkutano huo kuendelea kuimarisha na kudumisha ushirikiano uliopo katika Jumuiya, huku akibainisha kuwa kutokana na ushirikiano huo umeziwezesha nchi Wanachama kuweza kuhimili misukosuko inayosababishwa na kuyumba kwa uchumi wa dunia ikiwemo ongezeko la bei za bidhaa muhimu kama vile chakula.
Miongoni mwa ajenda muhimu zinazotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huo wa 25 wa Wakuu wa Nchi ni pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC, kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya ushuru (Non-Tariff Barriers – NTBs), kukubaliana kuhusu kanuni ya uchangiaji wa michango ya Jumuiya, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta za utalii, miundombinu na nishati.
Kwa sasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi wanachama nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia, ikiwa na jumla ya idadi ya watu inayokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 300 na pato la pamoja la uchumi (GDP) linalokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 300.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ukijumuisha Naibu Mawaziri kutoka sekta mbalimbali wakiwemo; Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde Naibu Waziri Fedha, Mhe. Regina Ndege Qwaray, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mhe. Dennis Lazaro Londo Naibu Waziri Viwanda na Biashara na Viongozi wengine Waandamizi wa Serikali.






No comments:
Post a Comment