
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa kushirikiana na Benki ya NMB, wamezindua rasmi huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki kutoka Benki ya NMB kupitia Mfumo wa NeST. Hatua hii inatarajiwa kuongeza uwazi, kasi na usalama katika michakato ya zabuni za umma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika leo, Machi 5, 2026, katika Ofisi za Makao Makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, amesema kusomana kwa Mfumo wa NeST na mifumo ya kibenki ni mapinduzi makubwa katika usimamizi wa ununuzi wa umma nchini, yaliyoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameongeza kuwa huduma hiyo itawezesha dhamana za zabuni zinazotolewa na NMB kuthibitishwa moja kwa moja kupitia NeST bila taasisi nunuzi kulazimika kuwasiliana na benki kwa njia ya barua kama ilivyokuwa awali ili kuhakiki uhalali wake.
“Mzabuni ataingiza namba ya dhamana aliyopewa na benki kwenye mfumo wa NeST, na mfumo utaivuta dhamana hiyo moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi. Hatua hii imeondoa kabisa mianya ya kughushi na imeongeza ufanisi katika mchakato wa zabuni,” amesema Bw. Simba.
Bw. Simba ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kujenga uchumi wa kidijitali na kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, amesema kupitia mfumo huo PPRA na NMB watafanya uhakiki wa Bank Guarantee pamoja na akaunti ya muomba zabuni na kutoa majibu papo hapo, huku mfumo huo ukilenga kurahisisha mchakato na kuboresha ufanisi wa utendaji kazi kwa wataalamu wa Ununuzi na Ugavi.
“Leo tunazindua rasmi suluhisho la ‘Digital Bank Guarantee Confirmation’ kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ambalo linaruhusu shughuli za ununuzi wa umma kuanzia usajili, zabuni, mikataba hadi malipo kufanyika kupitia mfumo wa NeST,” amesema Bi. Zaipuna.
Mfumo wa NeST umeunganishwa na mifumo 21 hadi sasa tangu ulipoanza kufanya kazi rasmi Julai 1, 2023.


No comments:
Post a Comment