
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania, Dkt. Anna Makakala, amesema maendeleo jumuishi si hisani, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma katika shughuli zote za maendeleo ikiwemo kushiriki katika maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
Dkt. Makakala ametoa kauli hiyo Machi 5, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema haki na usawa wa kijinsia vinapaswa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, akisisitiza kuwa Taifa haliwezi kufikia malengo yake ikiwa nusu ya rasilimali watu, hususan wanawake, itaachwa nyuma.
“Ukimuwezesha mwanamke familia inaimarika, na familia ikisimama imara basi Taifa nalo linaimarika,” amesema Dkt. Makakala.
Aidha, amesema uwakilishi sawa katika nafasi za maamuzi husaidia kuleta maamuzi sahihi na kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo viwanda na biashara. Kutokana na hilo, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu kwa wasichana.
Pia ameitaka jamii kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wasichana kufikia ndoto zao, ikiwemo kupinga ndoa za utotoni na kupiga vita unyanyasaji pamoja na ukatili wa kijinsia.
Amesema mwanamke anayefanyiwa ukatili wa kijinsia hushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na ujenzi wa Taifa.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa kupunguza pengo lililopo kati ya wanawake na teknolojia kwa kuwajengea uwezo wa kidijitali ili waweze kunufaika na fursa za maendeleo ya kidijitali, pamoja na kutengeneza bajeti zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Aidha, amehimiza kuwashirikisha wanawake kikamilifu katika uchumi wa kijani na fursa zinazotokana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Razack Lokina, amesema siku hiyo ni ya kihistoria kwa chuo hicho kwani maadhimisho hayo hayaadhimishi tu wanawake bali pia yanatambua mchango wao kama injini ya ukuaji wa uchumi.
Prof. Lokina amesema kauli mbiu ya mwaka inayosema “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050” inaonesha umuhimu wa kuwapa wanawake nafasi sawa katika maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa ni vigumu kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 bila ujumuishaji wa wanawake, kwani pale ambapo wanawake wanaachwa nyuma, hata maendeleo hubaki nyuma.
Ameongeza kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kitaendelea kushirikiana kwa karibu na Kitengo cha Jinsia pamoja na wanawake kwa ujumla ili kuhakikisha chuo hicho kinakuwa mfano wa kuigwa kwa vyuo vingine nchini katika kutoa fursa sawa kwa wanawake.
Naye Mratibu wa Kitengo cha Jinsia katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Lily Makalanga, akielezea historia ya Siku ya Wanawake Duniani, amesema maadhimisho hayo yalianza mwaka 1908 baada ya wanawake zaidi ya 15,000 kuandamana kudai nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kazi.
Amesema tarehe 8 Machi ilianza kuadhimishwa rasmi baada ya mgomo mkubwa wa wanawake uliofanyika mwaka 1917 nchini Urusi.
“Wanawake tuna wajibu wa kukaa na kutafakari fursa nyingi zilizopo nchini na kuona namna ya kuzitumia kuitumikia Taifa. Mwanamke ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Makalanga.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Kitengo cha Jinsia cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeandaa shughuli mbalimbali ikiwemo, kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakionekana kuwa ni ya wanaume zaidi.











No comments:
Post a Comment