
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema katika mkoa huo kuna changamoto ya uzalishaji,usafirishaji na biashara pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na wahusika wakubwa ni kundi la vijana katika eneo hilo.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo Machi 28,2025 alipokuwa kwenye Kongamano la Vijana la kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya tukio lililofanyika Jijini Dodoma.
"Dawa za kulevya zinazozalishwa ni bangi, na zinalimwa kwenye mazingira yenye vyanzo vya maji na ndani ya hifadhi zetu, dawa zingine kama mirungi, Kokeini nk" alisema.
Amesema pia kwa hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la Matumizi ya dawa tiba zenye Asili ya kulevya ambazo huchepushwa na kwenda kutumika kama kujistarehesha, na vijana wengi hasa wa kike kuingia kwenye matumizi ya Bangi aina ya Skanka.

Naye Afisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bi. Anna Tengia amesema kwa mujibu wa Sensa ya makazi ya mwaka 2022, Idadi kubwa ya vijana ni Milioni 21.3 na ndio kundi kubwa linaloongoza kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kuanzia umri wa miaka 13-35.
"Tuko sahihi kutoa elimu kwa vijana wa kitanzania kwa sababu ni kundi ambalo lipo hatarini zaidi kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya nchini" alisema Anna.
Aidha, Amesema kundi hilo la vijana linatumia zaidi dawa za kulevya aina ya Bangi na Skanka, hivyo mtu akitumia skanka inakwenda kuamsha magonjwa ya akili.
"Tukiwa kama vijana wa Tanzania tukatae madawa ya Kulevya ili tuweze kutimiza ndoto zetu na malengo yetu.
"Madhara ya dawa za kulevya ni makubwa yapo ya kiafya,kijamii, kiuchumi,kidiplomasia, kimazingira lakini vile vile kisiasa" alisema Anna.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Taifa Forum Bw. Charles Warioba, amesema kongamano hilo ni la pili kulifanya na limekuwa kongamano pekee na la kitofauti pia kutokana na mwitikio mkubwa wa watu wengi zaidi jijini Dodoma.






No comments:
Post a Comment