TANESCO YAONGEZA UZALISHAJI UMEME MARA MBILI NDANI YA MIAKA MINNE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, March 26, 2025

TANESCO YAONGEZA UZALISHAJI UMEME MARA MBILI NDANI YA MIAKA MINNE



Na Okuly Julius _DODOMA


Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema hali ya uzalishaji umeme kwenye Gridi ya Taifa imeongezeka mara mbili zaidi baada ya kutekeleza miradi ya ufuaji umeme maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo leo Machi 26, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Amesema kuwa hadi kufikia Februari 2025, uwezo wa mitambo ya kufua umeme kwenye Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya Megawati 3,697.71, wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme kwenye Gridi ya Taifa yalikuwa Megawati 1,908.

"Mwaka 2021, uwezo wetu wa kuzalisha ulikuwa Megawati 1,573.6, na sasa uzalishaji umeongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne," amesema Mhandisi Nyamo-Hanga.

Aidha, amesema kuwa TANESCO itaendelea kutekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji, na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika. Miradi inayoendelea ya uzalishaji ni pamoja na:

Malagarasi – MW 49.5

Kakono – MW 87.8

Kishapu Solar (Awamu ya Pili) – MW 100

Ruhudji – MW 358

Rumakali – MW 222




Pia, amesema kuwa TANESCO itaongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na makaa ya mawe.

Vilevile, Tanzania imeanza utekelezaji wa mradi wa nishati ya jotoardhi, ambapo mashine ya kuchoronga miamba (rig) inaendelea kufanya kazi katika eneo la Ngozi, Mbeya. Tafiti za awali zinaonyesha kuwa eneo hilo linaweza kuzalisha umeme wa Megawati 70.


MIKAKATI YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA UMEME


Mhandisi Nyamo-Hanga amesema kuwa TANESCO inaendelea kuimarisha miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuendana na ongezeko la mahitaji ya umeme nchini na kuunganisha Gridi ya Taifa na nchi za Uganda, DRC, Malawi, na Msumbiji.

Pia, shirika hilo linakamilisha miradi ya kusafirisha umeme ikiwemo:

Sumbawanga – Katavi – Kigoma

Mkuranga – Mtwara kupitia Kibiti na Somanga Fungu

Chalinze – Segera (400KV), Segera – Same – Arusha (400KV)

Segera – Tanga (220KV), Chalinze – Bagamoyo (220KV)

Chalinze – Kinyerezi – Mkuranga (400KV)




Aidha, TANESCO inaendelea kujenga miradi ya usambazaji umeme ili kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa sekta za madini, kilimo, na viwanda.


MPANGO WA KITAIFA WA NISHATI TANZANIA


Serikali ya Tanzania ilishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati (African Heads of States Energy Summit) uliofanyika Januari 27-28, 2025, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, viongozi wa Afrika walijadili mikakati ya kuhakikisha watu milioni 300 wanapata umeme ifikapo mwaka 2030. Pia, Tanzania ilizindua Mpango wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact 2025-2030), ambao unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme kutoka asilimia 78.4 hadi kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.

"Mafanikio haya yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya umeme nchini, na tunajivunia kuwa wananchi sasa wanapata umeme wa uhakika," amesema Mhandisi Nyamo-Hanga.

Shirika linaendelea kutekeleza miradi na maboresho mbalimbali ya miundombinu ya umeme nchini ili kuhakikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwapatia Watanzania umeme wa uhakika inafikiwa.


No comments:

Post a Comment