TANI 150 ZA VIFUNGASHIO VISIVYOKIDHI VIGEZO VYATEKETEZWA - DKT. SEMESI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 24, 2025

TANI 150 ZA VIFUNGASHIO VISIVYOKIDHI VIGEZO VYATEKETEZWA - DKT. SEMESI


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)Dkt. Immaculate Semesi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.


Na Okuly Julius _Dodoma


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Semesi,amesema zaidi ya tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa, na kuteketezwa kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Dkt. Semesi, ameyasema hayo leo Machi 24,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita

Amesema kaguzi 178 zilifanyika katika maeneo ya uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki, ambapo maeneo 57 yalibainika kuwa na makosa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Suala la udhibiti wa vifungashio vya plastiki ni jukumu la kila mmoja wetu. Tunapaswa kushirikiana ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Dkt. Semesi.

Ili kuongeza uelewa wa umma, Baraza limeandaa vipindi 88 vya uhamasishaji kupitia vyombo vya habari pamoja na mikutano 20 ya wadau kuhusu madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

Aidha, Dkt. Semesi amesema kuwa Baraza limesajili jumla ya miradi 8,058, ambapo 5,784 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira.

“Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho ya masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika taarifa hizo,” alieleza.

Kwa mujibu wa NEMC, miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira, ambapo 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vingine vikiwa ni vyeti vya kubadili masharti (169), vyeti vilivyohamishwa umiliki (552), vyeti vya muda (PEC) 53, na cheti kimoja cha kurudishwa (certificate of surrender).

Katika kuhakikisha ufanisi wa usimamizi wa mazingira, Baraza lilianzisha mfumo wa kielektroniki wa usajili wa miradi ya TAM. Kabla ya mfumo huo, miradi 900 ilikuwa inasajiliwa kwa mwaka, lakini baada ya kuanzishwa kwake, Baraza sasa linasajili zaidi ya miradi 2,000 kwa mwaka.

Dkt. Semesi alibainisha kuwa kati ya mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Baraza limesajili Wataalam Elekezi wa Mazingira 1,023 na kutoa vyeti vya utendaji kwa wataalam 503 waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili na Utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira za mwaka 2021.

“Jumla ya kaguzi 9,606 zilifanyika, huku malalamiko 1,483 yakishughulikiwa, hasa katika eneo la kelele na mitetemo. Uchafuzi wa mazingira ulidhibitiwa katika miradi mikubwa yenye viashiria hatarishi, ambapo programu 50 za elimu na vipindi 75 vya uhamasishaji viliandaliwa,” alisema.

Aidha, Baraza limetoa vibali 781 kwa wafanyabiashara mbalimbali, huku nyaraka 1,477 za ufuatiliaji zikitolewa. Kati ya hizo, 1,089 zilirejeshwa na kufanyiwa mapitio, ambapo ilibainika kuwa tani 165,834 za taka hatarishi zilifuatiliwa kwa mafanikio kote nchini.

Baraza limesisitiza kuwa litaendelea kuhakikisha sheria za mazingira zinatekelezwa kikamilifu ili kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na plastiki zisizokidhi viwango.

No comments:

Post a Comment