UWEZO TANZANIA NA RELI AFRICA WAANDAA MKUTANO WA TATHMINI YA MRADI WA STADI ZA MAISHA NA MAADILI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 24, 2025

UWEZO TANZANIA NA RELI AFRICA WAANDAA MKUTANO WA TATHMINI YA MRADI WA STADI ZA MAISHA NA MAADILI



Na Okuly Julius_ DODOMA


Shirika la UWEZO TANZANIA, kwa kushirikiana na RELI Africa (Mtandao wa Elimu Kikanda), limeandaa mkutano muhimu wa tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa Stadi za Maisha na Maadili.

Mkutano huo umehusisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, walimu, na wazazi, kwa lengo la kujadili maendeleo yaliyopatikana na kupanga hatua za mbele kwa mwaka 2025.

Akizungumza katika mkutano huo leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa UWEZO TANZANIA, Baraka Mgohamwende, amesema kuwa mradi huo wenye lengo la kukuza na kulea stadi za maisha na maadili ulianza mwaka 2021 kwa kufanya tafiti, ambazo zilionesha kuwa vijana wengi katika Afrika Mashariki wanakosa ujuzi wa kutosha kuhusu stadi za maisha na maadili.

Mgohamwende amefafanua kuwa kufuatia matokeo hayo, jitihada za uhamasishaji kwa wazazi na walimu zilifanyika katika wilaya sita nchini mwaka 2024, kwa lengo la kukuza stadi hizo kwa watoto.

"Katika mkutano wa leo, washiriki watajadili taarifa ya utekelezaji wa jitihada hizo na kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2025, ambao utajikita katika kuongeza uhamasishaji kwa wazazi na walimu ili kuimarisha stadi za maisha na maadili miongoni mwa watoto," amesema Mgohamwende.

Ameongeza kuwa jamii kwa muda mrefu imekuwa ikifurahia matokeo ya kitaaluma ya wanafunzi, kama kupata Division 1 au Alama A, lakini haitilii mkazo mchango wa watoto hao katika jamii baada ya kumaliza shule.

"Tafiti zinaonesha kuwa vijana wengi wakimaliza shule hawana mchango katika jamii. Kwa Tanzania Bara na Visiwani, utafiti huu umefanyika katika wilaya 35 na kuwafikia vijana 17,000, ambapo ni asilimia 8 tu ya vijana ndio walioonesha kuwa wanaweza kutatua changamoto zao wenyewe," amesema Mgohamwende.

Ameeleza kuwa UWEZO TANZANIA, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inatafuta njia bora za kupandikiza stadi za maisha kwa vijana ili waweze kujisaidia na kuwa na mchango chanya katika jamii.

"Moja ya mbinu tunazotumia ni kushirikiana na wizara mtambuka ili kuboresha sera zinazohusu malezi kwa vijana, pamoja na kuandaa mifumo ya kupima uwezo wa vijana wa kuwasiliana na kushirikiana katika jamii. Tunashirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania na wadau wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kuandaa mbinu sahihi za kupima ubobevu wa stadi hizi," ameongeza Mgohamwende.

Kwa upande wake, Digna Mushi, ambaye ni Kiongozi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (RELI), amesema kuwa kupitia ripoti ya utafiti huo, watatengeneza mikakati madhubuti kuhakikisha kuwa vijana na watoto wanapata ujuzi wa kushirikiana na kuwasiliana ili waweze kujitatulia changamoto zao.

"Mradi huu umeangazia namna walimu na wazazi wanavyowatengeneza watoto wenye uwezo wa kushirikiana na kuwasiliana. Sasa kupitia mkutano huu, tutachakata maoni na kuweka mkakati mahususi wa kufanikisha lengo hilo," amesema Bi. Digna.


Naye Mahmudi Ngamange, Afisa Ubora wa Elimu wa Shirika la SAWA, amesema kuwa mradi huo umeleta mafanikio makubwa katika Wilaya ya Mvomero, Morogoro, hasa katika kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

"Kwa mfano, kupitia mradi huu tuliwafundisha wazazi nao wakawafundisha watoto wao namna ya kuchunga mifugo bila kuharibu mashamba ya wakulima. Mafunzo haya yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro baina yao," amesema Ngamange.

Mkutano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuboresha elimu ya stadi za maisha na maadili nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.




No comments:

Post a Comment