Kongwa, Dodoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kupitia Mradi wa RISE - Uondoaji wa vikwazo vya barabara umekamilisha Mradi wa matengenezo ya Barabara ya Songambele - Banyibanyi yenye urefu wa Km 10.
Barabara hiyo inayounganisha Kata za Songambele na Hogoro inatajwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kata hizo wanaojishughulisha na kilimo cha mazao mchanganyiko na ufugaji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele Bw. Said Matonya amesema kuwa moja ya manufaa ya kukamilika kwa barabara hiyo ni kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Kata za Songambele na Hogoro.
"Barabara hii imesaidia maeneo yetu mengi ya huduma za jamii, kwa mfano kilimo ambacho hufanyika maeneo ya magharibi kule kwa hiyo mazao yanasafirishwa kwa urahisi na kufika masokoni kwa wakati' amebainisha
Kwa upande wake Bibi Dora Christopher Samira Mkazi wa Kijiji cha Songambele amesema hapo awali walipata changamoto hasa kipindi cha mvua ambapo watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule, watu wa maeneo ya Masena walikuwa wanashindwa kuzifikia huduma za kijamii lakini baada ya mradi huo huduma nyingi sasa zinafikiwa kwa urahisi ikiwemo huduma ya afya, amefafanua Bibi Dora.
Mzee Ivan Maswaga Wenga mkazi wa Kijiji cha Songambele kwa upande wake anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea barabara kwani barabara hiyo ilikuwa inawazuia wanafunzi kwenda shule ya Msingi Ndachi na shule ya sekondari Mnywange hivyo ni matumaini yake Sasa kuwa barabara hiyo itawarahishia vijana wao kupata elimu kwa urahisi.
Naye, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kongwa Mhandisi Boniface Mandi amesema kuwa Mradi huo umehusisha matengenezo ya barabara Km 10 na ukarabati wa makavati matano na unapita katika vijiji vitatu Songambele, Masena na Banyibanyi na umekamilika kwa 100%.
No comments:
Post a Comment