
Na MWANDISHI WETU _ DODOMA
Serikali imewaagiza wakurugenzi, wenyeviti na mameya wa halmashauri nchini kufanya tathimini ya kwanini halmashauri zao hazijafikia malengo ya ukusanyaji wa kodi za majengo na ushuru wa mabango.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Tamisemi Dk Festo Dugange leo Jumatano, Machi 12,2025 kwa niaba ya Mchengerwa wakati akifunga mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT).
Aidha, Mchengerwa amesema eneo la ukusanyaji kodi ya majengo na ushuru wa mabango bado halmashauri hazijafanya vizuri ambapo kwa sasa ni asilimia 38 hivyo kuwataka kufanya tathimini ni kwanini hawajafika malengo kusudiwa na kwamba ifikapo Juni mwaka huu wawe wamefikia asilimia 90.
Pia, amewataka kusimamia utoaji huduma kwenye sekta za afya ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa serikali kuhusu huduma mbaya na lugha mbaya kwa wateja na kuweka mikakati ya kudhibiti fedha za uchangiaji huduma za afya.
Amesema halmashauri hazijawa makini katika ukusanyaji wa kodi ya majengo na ushuru wa mabango na kuwataka watakapofika katika maeneo yao kufanya vikao vya kufanya tathimini ni kwanini halmashauri zao hazijafikia malengo ya ukusanyaji wa kodi hizo.
Aidha, Mchengerwa amewataka kwenda kufanya tathimini katika halmashauri zao juu ya ukusanyaji wa mapato na kama kuna mianya ya upotevu na wachukue hatua za kisheria za haraka kwa kuwapeleka mahakamani wataalam ambao wamejiridhisha kuwa wamehusika na upotevu wa mapato.
“Mkajiridhishe kama wataalam wamehusika na upotevu wa mapato kwa kutumia risiti feki au kwa utaratibu wowote. Tunataka kuona hatua za kisheria zinachukuliwa haraka iwezekanavyo na zionekane kupitia vyombo vya habari kuwa wamepelekwa mahakamani na Tamisemi tuipate taarifa hiyo,”amesema.
“Tuhakikishe sheria inachukua mkondo wake kama kuna mkuu wa idara, mkuu wa kitengo ama mtaalam aliyehusika kupoteza mapato yetu katika halmashauri tuhakikishe tunaona kupitia vyombo vya habari wako katika mikononi ya sheria na hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao,”amesema.
Amesema kutokana na unyeti wa kazi zao ni lazima wadhibiti upotevu wa mapato ya ndani ya halmashauri na kuwa kuna maeneo ambayo ufujaji wa mapato upo kwa kutumia risiti feki.
Ametoa mfano wa Halmashauri ya Meatu mkoani Simiyu ambapo kuna watu wanatumia flashi inayotengeneza risiti na kuunganishwa na katika mfumo wa risiti za kieletroniki za Pos ili kukidhi matakwa ya wanaotengeneza.
Amesema jambo hilo halikubaliki na kumtaka Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meatu kwenda kulidhibiti jambo hilo haraka.
Awali Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Atupele Mwambene amesema katika mkutano huo Tamisemi imeutumia kujua changamoto za kiutendaji ili kuzitatua.





No comments:
Post a Comment