
Na Okuly Julius _ DODOMA
Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuhakikisha wanaishirikisha jamii hususani wataalamu wa sekta ya Maji wastaafu, wanapofanya tafiti za kina za kugundua vyanzo vipya vya maji.
Aweso ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa Ziara ya kukagua miradi ya Maji inayosimamiwa na Mamalaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (DUWASA) katika eneo la Nala, Chihoni.
"Ni muhimu kuwatumia wazee wastaafu katika kutafiti na kubaini maeneo yenye maji ya kutosha bila kuwasahau wanajamii kwani kuna watu wenye uwezo wa kugundua maeneo yenye asili ya maji na sisi kama watalaam tukipima tunapata maji,"amesema Aweso
Aweso amesema kuwa jitihada ni kubwa zinayofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maji ya kuhakikisha kuwa wakazi wa Jiji la Dodoma wanapata maji safi na salama na moja ya jitihada hivyo ni kubaini na kupata vyanzo vipya vya maji.

Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Mhe Antony Mavunde amesema kukamilika kwa miradi ya uchimbaji wa visima vya maji pembezeno mwa mji itasaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya Nala,Chihoni,Segu na maeneo ya Viwanda.
Aidha amemuomba Waziri wa Maji kuendelea kufanya utafiti wa kina ili kuongeza vyanzo vipya vya maji ili kupunguza adha ya maji katika jiji la Dodoma.
"Mimi naendelea kukuomba Mhe.Aweso kuwa yaani mwisho wa matatizo ya maji katika jiji hili ni kufanyika kwa utafiti wa kina utakaobaini yalipo maji ya uhakika na kuchimba visima vingi na kuhakikisha wananchi wa jiji la Dodoma wanapata maji,"ameeleza Mavunde

Awali akisoma taarifa ya Miradi ya maji ya Nala na Amani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma [DUWASA] Mhandisi Aron Joseph amesema miradi hiyo ni mpango wa muda mfupi wa kuondoa adha ya maji katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dodoma.
Mhandisi Aron amesema miradi hiyo itasaidia kuongeza hali ya uzalishaji maji huku akisema zaidi ya Bilioni 3 zimetumika kutekeleza mradi wa maji Nala wakati Bilioni 41 kwenye Mradi wa uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa mji katika eneo la Amani
Nao baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira DUWASA kwa kuwachimbia visima hivyo vya maji kwani awali kabla ya uwepo wa miradi hiyo kutekelezwa katika maeneo hayo walikuwa wanatumia muda mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama.



No comments:
Post a Comment