
Na Mwandishi Wetu _ Dodoma
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema kuwa idadi ya taasisi za umma zilizopata hati safi imeongezeka hadi kufikia 220 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jambo linaloashiria kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa fedha serikalini.
Amebainisha hayo leo jijini Dodoma Aprili 16 ,2025 wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambapo ameeleza kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya taasisi nyingi sasa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ukaguzi na uwajibikaji.
Hata hivyo, CAG Kichere amesisitiza kuwa bado yapo maeneo mengi yenye changamoto, hasa katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanakuwa na tija na thamani halisi kwa wananchi.
“Ingawa tumeona mafanikio ya hati safi, bado tunakutana na changamoto kwenye matumizi yasiyoleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi. Hili ni eneo linalohitaji maboresho zaidi,” amesema Kichere.
Akizungumzia kuunganishwa kwa baadhi ya mashirika ya umma, CAG amesema kuwa ni mchakato unaoendelea na kwamba ofisi yake inaendelea kuishauri Serikali kuhusu umuhimu wa kuimarisha bodi za usimamizi na ufanisi wa menejimenti.
Lengo ni kuhakikisha mashirika yanayopata hasara kwa sasa yanaweza kuanza kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza mapato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Halima Mdee, amesema kuwa kamati yao imepokea kwa uzito mkubwa taarifa hiyo ya ukaguzi, na sasa wanaanza rasmi mchakato wa kibunge wa kuchambua na kujadili taarifa hiyo.
Ameeleza kuwa eneo la Serikali za Mitaa ni nyeti sana kwa sababu ndiko waliko wananchi wengi, hivyo ni lazima kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi, na kwa kuzingatia mipango ya maendeleo.
“Taasisi 220 kupata hati safi ni hatua nzuri, lakini tunapaswa kujiuliza kama hali halisi inadhihirisha matumizi bora ya fedha. Ndiyo maana tunakwenda mbele zaidi katika kuhakikisha tunapima uhalisia wa taarifa hizi kwa maslahi ya wananchi,” amesema Mdee.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Mary Masanja, alieleza kuridhishwa kwake na namna CAG anavyotekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu.
Ameongeza kuwa uwazi wa taarifa hizi unasaidia kuijengea Serikali imani kwa wananchi na wawekezaji.
“Tunampongeza CAG kwa kazi kubwa anayofanya. Ripoti hizi ni nyenzo muhimu kwa wabunge, kwa Serikali, na kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinafanya kazi iliyokusudiwa,” amesema Masanja.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Ofisi ya CAG ipo kwenye majadiliano na Bunge kuhusu kuanza kujadili taarifa hizi mapema zaidi, ambapo badala ya mwezi Novemba kama ilivyozoeleka, mapendekezo yaliyopo ni kufanya majadiliano haya kuanzia mwezi Juni, ili kuwezesha utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti kufanyika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment