
Na Okuly Julius _ DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imetoa wito kwa wananchi wote kushirikiana katika kuhakikisha watoto wa Tanzania wanalelewa katika mazingira salama, yenye upendo na fursa za maendeleo.
Wito huo umetolewa leo Aprili 9,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto Anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani, yatakayofanyika kitaifa tarehe 12 Aprili 2025 katika Ukumbi wa VETA, Mkoani Mtwara.

Dkt. Gwajima, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, familia na jamii kwa ujumla katika kutatua changamoto zinazowasukuma watoto kuishi na kufanya kazi mitaani.
Kauli mbiu ya mwaka huu “Imarisha Ushirikiano Kuzuia Mtoto Kuishi Mtaani” inalenga kuhamasisha mshikamano wa kitaifa katika kulinda haki na ustawi wa mtoto.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na Waziri Gwajima, imebainika kuwa kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, jumla ya watoto 8,372 waliokuwa wakiishi na kufanya kazi mitaani wameokolewa na kupatiwa huduma mbalimbali. Kati yao, 5,812 waliunganishwa na familia zao, 1,056 wapo katika makao ya watoto na nyumba salama, huku wengine wakipelekwa kwa walezi wa kuaminika au kupatiwa elimu na mafunzo ya ufundi.
Aidha, serikali imeanzisha kampeni ya kitaifa ya “Kumuokoa Mtoto Kutoka Mtaani” iliyoanza rasmi tarehe 07 Aprili 2025.
"Kampeni hii inatekelezwa kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii, Polisi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali, ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha mtoto anapata ulinzi wa kutosha na kurejeshwa katika mfumo rasmi wa malezi ya familia au taasisi maalum,"ameeleza Dkt.Gwajima
Mbali na hilo, Dkt.Gwajima amesema serikali imeweka mikakati mbalimbali kupitia modeli ya “Close the Tap” inayolenga kuzuia kabisa mianya inayosababisha watoto kuingia mtaani kwa kushughulikia changamoto za kifamilia na kiuchumi.
Dkt.Gwajima amesma katika kuelekea kilele cha maadhimisho, kutafanyika midahalo ya ana kwa ana pamoja na mijadala ya mtandaoni kujadili namna bora ya kudhibiti tatizo hili. Mdahalo mkubwa utafanyika tarehe 11 Aprili 2025 katika Kata ya Chikongola, Mtwara ukihusisha wananchi, viongozi na wadau mbalimbali.
Amesisitiza kuwa watoto wanaoishi mitaani ni sehemu ya jamii yetu, na ni jukumu letu sote kuhakikisha wanapata maisha bora, elimu na ulinzi wa haki zao. Wananchi wa Mtwara na vitongoji mnaombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha maadhimisho haya tarehe 12 Aprili 2025, VETA Mtwara.




No comments:
Post a Comment