
Na WMJJWM - DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, ameongoza ufunguzi wa kikao muhimu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024, akitoa msisitizo kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
Akihutubia washiriki katika wa kikao hicho kilichojumuisha wataalamu na watendaji kutoka Wizara mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali na ya kimataifa pamoja na wadau wanaotekeleza afua za kupinga ukatili nchini kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 23, 2025 Dkt. Jingu alieleza kuwa licha ya mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa kama vile kuimarika kwa huduma kwa waathirika wa ukatili na kuongezeka kwa uelewa wa jamii bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka na umakini.
"Changamoto kama umasikini wa kaya, ndoa na mimba za utotoni, ukatili wa kingono na kisaikolojia bado ni tatizo kubwa. Tunahitaji ushirikiano wa kweli baina ya sekta zote ili kuhakikisha MTAKUWWA inatekelezwa kikamilifu," alisema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na taasisi nyingine kuhakikisha lengo la kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 linafikiwa.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Nandera, amewataka washiriki kwenda kusimamia vizuri majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo na majumuisho ya kikao hicho ili kutekeleza adhma ya MTAKUWWA na kufikia malengo yake ya kutokomeza ukatili kwani utekelezaji thabiti wa mpango huu unahitaji dhamira ya dhati, uwajibikaji, na usimamizi makini kutoka kwa kila mdau katika ngazi zote kuanzia Serikali Kuu hadi mitaani.
Washiriki wa kikao hicho waliupongeza uongozi wa Wizara kwa uongozi imara na mwelekeo mzuri katika kuratibu MTAKUWWA. Walitoa shukrani kwa uwasilishaji wa taarifa na majadiliano yenye tija, huku wakiahidi kwenda kutekeleza maelekezo yote kwa bidii, uwazi na ushirikiano ili kuhakikisha jitihada za kutokomeza ukatili zinazaa matunda katika jamii zao.










No comments:
Post a Comment