BUNGE LAENDELEA KUDHAMINI ELIMU KWA VITENDO KUPITIA BUNGE MARATHON 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 12, 2025

BUNGE LAENDELEA KUDHAMINI ELIMU KWA VITENDO KUPITIA BUNGE MARATHON 2025




Na Okuly Julius _ DODOMA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amewaongoza Mawaziri, Wabunge na Wananchi katika mbio za hisani za Bunge Marathon 2025, zilizoandaliwa kwa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wavulana ya kidato cha tano na sita.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alisema shule hiyo mpya itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 300, na itajumuisha mabweni, maktaba ya kisasa, bwalo kubwa la chakula, viwanja vya michezo pamoja na nyumba za walimu.


"Ujenzi wa shule hiyo itakayokuwa na uwezo wa kusajili wanafunzi wasiopungua 300 hadi 350 kwa mwaka utagharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu,"ameeleza Majaliwa

Shule hiyo ya kidato cha tano na sita itajengwa katika eneo la Kikombo, Jijini Dodoma karibu kidogo na shule ya wasichana iliyojengwa na wabunge wanawake 2020.

“Ninawapongeza sana Wabunge wenzangu kwa kuweka alama na kugusa maisha ya Watanzania na watoto wetu wa kiume watakaopata fursa ya kusoma katika shule hiyo.”

Amesema ujenzi wa shule hiyo ni mpango wa Bunge wa kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia suluhu Hassan katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu.

Shule hiyo ya bweni itakuwa maabara nne za biolojia, kemia, fizikia na jiografia, maktaba, bwalo la chakula, nyumba za walimu pamoja na viwanja vya michezo.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, alisema kuwa baada ya mafanikio ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wasichana, sasa Bunge linaendelea na ujenzi wa shule ya wavulana kama ishara ya kuonesha usawa wa kijinsia na dhamira ya kuwatunza na kuwaendeleza watoto wote wa Tanzania bila ubaguzi.

Dkt. Tulia alieleza kuwa mbio hizo za hisani pia zimetoa fursa kwa washiriki kujenga afya zao na kuungana kwa pamoja katika azma ya kulijenga taifa kupitia elimu.

“Bunge limeona umuhimu wa kujenga shule ya sekondari ya wavulana, na hii ni baada ya kuwa na shule ya Bunge ya wasichana. Watoto wote ni wetu, na ndio maana tukaona umuhimu wa hili. Nawashukuru washiriki wote kwa mchango wao katika ujenzi huu,” alieleza Dkt. Tulia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bunge Marathon 2025, Mheshimiwa Festo Sanga, alisema mbio za mwaka huu zimevutia washiriki zaidi ya elfu 4, ongezeko kubwa kutoka washiriki elfu 3 wa mwaka 2024, jambo ambalo linaonesha jinsi ambavyo wananchi wanazidi kuhamasika kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo kupitia Bunge Marathon.

“Sisi kama Bunge tumefarijika sana kuona mwaka huu washiriki wameongezeka ukilinganisha na mwaka jana. Watu wamevutiwa, wamehamasika, na wamejitokeza kwa wingi. Mbio hizi zimevuka matarajio yetu, na tunajivunia mafanikio haya,” amesema Sanga.

Bunge Marathon imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuchangisha fedha kwa ajili ya maendeleo ya elimu huku likiwaunganisha Wabunge, wananchi, na taasisi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Visiwani.








No comments:

Post a Comment