
KANUNI ZA MAADILI YA UCHAGUZI WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI, 2025
3.2 Mambo Yasiyotakiwa Kufanywa na Serikali Wakati wa Uchaguzi
Serikali haipaswi kufanya mambo yafuatayo wakati wa uchaguzi:
(a) Kuingilia au kuzuia isivyo halali mikutano iliyoitishwa na vyama vya siasa au wagombea kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi.
(b) Vyombo vya ulinzi na usalama kutumia mamlaka yake kukandamiza wagombea, wafuasi au chama chochote cha siasa.
Maelekezo: Vyombo hivyo vinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, haki na weledi.
(c) Kumhamisha mtumishi yeyote wa Serikali anayehusika na shughuli za uchaguzi mpaka mchakato wa uchaguzi ukamilike.
Maelezo ya ziada: Iwapo kuna ulazima wa kumhamisha mtumishi huyo, Serikali inapaswa kushauriana na Tume ya Uchaguzi.
3.3 Mambo Yasiyotakiwa Kufanywa na Watendaji wa Serikali Wakati wa Uchaguzi
Watendaji wa Serikali hawapaswi kufanya yafuatayo wakati wa uchaguzi:
(a) Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, na Wakuu wa Wilaya kuchanganya ziara za kikazi na shughuli za kiuchaguzi, na kutumia vyombo au watendaji wa Serikali kwa manufaa yao kisiasa.
(b) Kuanzia kipindi cha kampeni hadi kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, Mawaziri hawaruhusiwi:
(i) Kutangaza misaada au ahadi ya aina yoyote kupitia vyombo vya habari au kwa namna nyingine yoyote.
(ii) Kutoa ahadi za maendeleo ya jamii kama vile ujenzi wa barabara au usambazaji wa maji kwa lengo la kuungwa mkono kisiasa.
(iii) Kutumia madaraka au rasilimali za Serikali kwa shughuli za kampeni kwa manufaa ya chama au mgombea yeyote.
(c) Waziri au afisa mwandamizi yeyote wa Serikali kumwita msimamizi wa uchaguzi kwa lengo la kujadili au kutoa maelekezo kuhusu masuala ya uchaguzi, kuanzia kipindi cha kampeni hadi kutangazwa kwa matokeo.
(d) Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wa Serikali kuingia katika vituo vya kupigia, kuhesabia au kujumlishia kura.
Isipokuwa: Wanaruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura kwa madhumuni ya kupiga kura tu.
No comments:
Post a Comment