MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJISAFI NALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 26, 2025

MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJISAFI NALA



Na Okuly Julius _ DODOMA


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amewataka wananchi wa Kata ya Nala, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa na Kiongozi huyo wakati akiweka jiwe la msingi katika Mradi wa Majisafi Nala, mradi unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa gharama ya shilingi bilioni 3.4

Pia ameitaka DUWASA kuishirikisha jamii pindi changamoto ya maji inapotokea ili kuondoa taharuki na malalamiko kwa kukosekana kwa taarifa rasmi ya sababu zinazopelekea kutokuwepo kwa maji.

"Nitoe wito kwa wanachi wa Nala ,mradi huu umewekezwa fedha kwa ajili ya kuwasaidia nyinyi ili muondokane na adha ya maji sasa kazi yenu ni kuhakikisha mnautunza ili uweze kudumu,"amesisitiza Ussi


Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, alisema kuwa gharama ya awamu ya kwanza ya mradi ni shilingi bilioni 1.4, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 827 kimeshatumika.


Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, alisema eneo la Nala lilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hivyo utekelezaji wa mradi huo utasaidia sana wananchi wa eneo hilo.

Awamu ya kwanza ya Mradi wa Majisafi Nala imehusisha uchimbaji wa kisima kimoja, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 200,000, ujenzi wa nyumba ya mradi, ulazaji wa bomba la maji lenye urefu wa kilomita 7.8, ufungaji wa pampu, ukarabati wa tenki la zamani lenye ujazo wa lita 45,000, pamoja na ufungaji wa mifumo ya umeme.

Kauli Mbiu ya mwaka huu ya mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa ni "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa Amani na Utulivu"














No comments:

Post a Comment